Habari

Mkuu wa CIA kuhojiwa na bunge la Seneti Marekani, Sababu ya mauaji ya Khashoggi

Mkurugenzi wa shirika la ujasusi la Marekani Bi Gina Haspel atafanya mahojiano na wajumbe wa bunge la Congress juu ya mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi. Vyombo vya habari nchini Marekani vinaripoti kuwa bi Haspel atakutana na viongozi wa bunge la Seneti baadae leo Jumanne.

Kwa mujibu wa BBC, Mkurugenzi huyo hakuwepo wiki iliyopita wakati mawaziri wa mambo ya nje na ulinzi walipofanya mazungumzo na viongozi wa Seneti, kitendo ambacho kiliwakasirisha baadhi ya wajumbe wa bunge hilo.

Khashoggi aliuawa ndani ya ofisi za ubalozi mdogo wa Saudi Arabia jijini Istanbul, Uturuki Oktoba 2. Mwanahabari huyo alikuwa ni mkosoaji mkubwa wa sera za Saudia hususani mwanamfalme Mohammed bin Salman. Vyombo vya habari vya Marekani pia vimeripoti kuwa ripoti ya CIA juu ya mkasa huo inaonesha kuwa kuna uwezekano mkubwa kuwa bin Salman aliamuru mauaji hayo.

Tayari Saudia imewashitaki watu 11 juu ya mauaji hayo, lakini wanakanusha vikali juu ya uhusika wa bin Salman.

Vyombo vya habari nchini Marekani pia vinaripoti kuwa CIA wana ushahidi unaonesha kuwa bin Salman aliwasiliana kwa wa ujumbe nfupi wa simu ya mkononi na Saud al-Qahtani ambaye inadaiwa ndiye aliyeendesha operesheni ya mauaji ya Khashoggi.

Waziri wa mabo ya nje wa Marekani Mike Pompeo na waziri wa ulinzi James Mattis waliwaambia maseneta wiki iliyopita kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaomhusisha bin Salman na mauaji hayo. Rais wa Marekani Donald Trump amekuwa mstari wa mbele kumtetea bin Salman akidai kuwa ripoti ya CIA haikuhitimisha kinagaubaga kuwa mwanamfalme huyo aliamuru Khashoggi auawe. Bi Haspel pia anadaiwa kukasirishwa na kuvuja kwa ripoti ya CIA kwa vyombo vya habari.

Msimamo wa Seneti

Maseneta wengi, kutoka vyama vyote vya Republican na Democrats hawafurahishwi na msimamo wa Trump juu ya mauaji hayo, na hasira zao ziliongezeka zaidi baada ya bi Haspel kutohudhuria mahojiano ya wiki iliyopita. Kuonesha hasira zao, maseneta hao walipiga kura 63 kwa 37 mpango wa kusitisha usaidizi wa Marekani kwa Saudia na washirika wake kwenye vita nchini Yemen. Mpango kama huo uliwasilishwa bungeni mapema mwaka huu lakini ulitupiliwa mbali.

“Ni wakati sasa kuwatumia salamu Saudia kwa namna ambavyo wanavunja haki za binaadamu na kutengeneza janga kubwa nchini Yemen,” amesema Seneta Bob Mendez wa Democrat.

Seneta wa Republican Lindsey Graham amesema hatapiga kura kwenye muswada wowote mpaka pale bi Haspel atakapolieleza bunge la seneti ukweli wa mambo.

“Namna ambayo utawala huu umelishughulikia suala la Khashoggi haikubaliki kabisa,” amesema na kuongeza: “Mahojiano (ya wiki iliyopita) hayakunisaidia hata kidogo kuelewa mchango [wa bin Salman] katika mauaji ya Khashoggi.”

Jamal Khashoggi ni nani?

Akiwa mwanahabari mashuhuri, aliripoti habari kubwa kama uvamizi wa Usovieti nchini Afghanistan na kufanya mahojiano na Osama Bin Laden.

Kwa miongo kadhaa alikuwa na ukaribu na familia ya kifalme ya Saudia na pia aliwahi kuhudumu kama mshauri wa serikali. Hata hivyo alijitenga na utawala wa sasa na kuwa mkosoaji kisha kukimbilia nchini Marekani akihofia maisha yake mwaka jana. Akiwa Marekani alikuwa akiandika makala kila mwezi katika gazeti la Washington Post ambapo aliendeleza harakati zake za kumkosoa Mohammed bin Salman.

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents