Habari

Mkuu wa majeshi Uganda aungana na Bobi Wine kuanzisha chama kipya kumkabili Museveni

Aliyekuwa mkuu wa majeshi na rais wa chama kikuu cha upinzani cha FDC nchini Uganda, Jenerali Mugisha Muntu, ametangaza kuwa ataunda chama kipya cha kisiasa baada ya kukiaga chama hicho rasmi huku akitarajiwa kuungana na mbunge wa Kyadondo Mashariki, Robert Kyagulanyi (Bobi Wine).

Rais wa chama kikuu cha upinzani cha FDC nchini Uganda, Jenerali Mugisha Muntu

Kwa mujibu wa Shirika la habari la DW, Tamko hili la Mugisha Muntu linakuja siku mbili baada ya mkuu huyo wa zamani wa majeshi ya Uganda kujiondoa na kuzidisha mashaka kuhusu mpasuko katika chama hicho cha kiongozi mkuu wa upinzani, Kizza Besigye. Hata hivyo, amesisitiza kuwa nia yake kuu si kuwania urais kwa sasa lakini kujenga muundo thabiti kuleta mageuzi ya kisiasa Uganda.

Mbunge wa Kyadondo Mashariki, Robert Kyagulanyi (Bobi Wine).

Dalili za mpasuko katika chama cha FDC zilianza kudhihirika baada ya Mugisha Muntu kushindwa katika uchaguzi wa rais wa chama na Patrick Oboi Amuriat aliyeungwa mkono na kiongozi wa siku nyingi wa upinzani Dr. Kizza Besigye. Uchaguzi huo ulifanyika mwishoni wa mwaka jana.

Tangu wakati huo amekuwa akiendesha mikutano ya mashauriano na wafuasi wake sehemu mbalimbali za nchi. Aidha tabia ya wengi wa wabunge wakiongozwa na aliyekuwa kiongozi wa upinzani bungeni, Winnie Kizza, kuvunja mahusiano na rais mpya wa chama cha FDC ilikuwa ishara tosha kuwa hawangeunga mkono uongozi mpya wa chama hicho.

Hii ndiyo mojawapo ya sababu zilizompelekea rais huyo wa chama kuwafuta kazi wawakilishi wa upinzani kwenye kamati mbalimbali za bunge hata kabla ya awamu yao kukamilika. Kulingana na wadadisi wa kisiasa, hatua ya Muntu kujiondoa kutoka chama hicho ni pigo kubwa kwa FDC kwani kuna uwezekano wa wabunge wengi wa chama hicho kuhamia chama kipya anachokianzisha.

Katika kikao cha leo asubuhi na wanahabari, Jenerali Muntu amekanusha madai ya kumshawishi mwanasiasa na msanii mashuhuri, Bobi Wine, kujiunga naye hali inayopelekea ya yeye kuchelewa kuunda chama kipya. Lakini kwa mtazamo wa wengi wana matarajio kwamba msanii huyo ambaye ameleta joto jipya katika siasa za upinzani ataungana naye ili kuleta upinzani kwa chama tawala cha rais Museveni.

Kwa upande mwingine, kuna dhana kwamba migawanyiko katika vyama vya upinzani ni kielelezo kuwa wanasiasa wengi wanajitakia makuu na wala hawatangulizi maslahi ya taifa. Rais Museveni mwenyewe aliwahi kutamka kuwa vyama vya upinzani vitatokomea ifikapo mwaka 2021 kabla ya uchaguzi mkuu. Ndiyo maana baadhi ya watu wanahisi kuwa mipasuko katika vyama vya upinzani inatokana na harakati zake kufanikisha hilo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents