Siasa

Mmiliki Tabata Dampo atimuliwa kwa mawe

WAKATI wakazi wa Tabata Dampo, Ilala Dar es Salaam leo wanatakiwa kuachia eneo hilo, jana hali ilikuwa tete baada ya anayedai kumiliki eneo hilo kisheria, Kampuni ya Allied Cargo Freighters Limited kutimuliwa kwa mawe

Na Zamzam Abdul




WAKATI wakazi wa Tabata Dampo, Ilala Dar es Salaam leo wanatakiwa kuachia eneo hilo, jana hali ilikuwa tete baada ya anayedai kumiliki eneo hilo kisheria, Kampuni ya Allied Cargo Freighters Limited kutimuliwa kwa mawe.

Katika tukio hilo la aina yake ambalo mwandishi wa habari hizi alishuhudia, mmliki huyo alituma watu kwenda eneo hilo kuhakikisha wananchi hao wanaondoka kabla ya muda uliopangwa ambao ni leo, ambao walifika wakiwa wamepanda kwenye gari aina ya Landrover 110, Defender, ndipo wakazi hao walianza kuwavurumushia mawe na gari hilo kuondoka kwa kasi.

“Tulitaka kuwamaliza, hawawezi kuingia katika eneo letu ‘kutusanifu’ tumekwishasema kuwa hatutaondoka katika eneo hili hadi mahakama itoe uamuzi juu ya kesi hii “, alisema msemaji wa waathirika hao Bw.Taudhan Hariri.

Aliendelea kusema ” Pamoja na kujitapa katika vyombo vya habari kuwa watakuja kututoa, sasa tunawaambia kuwa tumeshaanza kujenga tena na tupo tayari kwa lolote leo tumejiandaa kama walivyojiandaa wao na tunasubiri mapambano,”alisema Bw. Hariri.

Alisema wanamshangaa msimamizi wa Kampuni hiyo Bw.John Nyange kwa kuidharau serikali na kusema kuwa fedha za fidia zilizolipwa kwa waathirika sio halali na kwamba mahakama ilishatoa uamuzi juu ya umiliki wa kiwanja hicho, jambo ambalo alidai kuwa si kweli na wala mahakama haijatoa uamuzi wowote katika kesi hiyo inayoendelea.

“Hapa kambini tuko watu zaidi ya 96 lakini tumeandaa watu wengine 300 kwa ajili ya kuja kutusaidia kukabiliana na hao wanaodai kuwa ndio wamiliki wa eneo hilo” alisema Bw. Hariri.

Juzi wamiliki wa kampuni ya Allied Cargo Freighters walidai kwamba tume iliyoundwa kuchunguza ubomoaji wa nyumba hizo ilizingatia zaidi maslahi binafsi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Abbas Kandoro na kushidwa kusimamia haki za pande zote mbili.

Msimamizi wa kampuni hiyo Bw. Nyange alikaririwa akisema katika mkutano wake na waandishi wa habari kuwa wananchi hao wanatakiwa kuondoka haraka katika eneo hilo kwani tayari wamelipwa fidia na kupewa viwanja eneo la Chanika Mbuyuni ili wao wahamie na kuendeleza shughuli zao.

“Tutaingia rasmi katika eneo hilo ili tuanze shughuli zetu kwa kuwa ni haki yetu kama raia kama serikali ilivyowasaidia wavamizi hao kuwalipa fidia tunaamini pia watasimamia ili waweze kuondoka” alisema.

Bw. Nyange alisema kwa tamko hilo, wanapenda kuutarifu umma kuwa kampuni imeteua kampuni nyingine ya majembe Action Mart and Court Brokers ya Dar es Salaam kusaidia katika zoezi la kuwaondoa wavamizi hao ikisaidiwa na vyombo vya dola.

Pamoka na Kampuni ya Allied Cargo kutoa saa 24 kwa wakazi hao bado wameendelea kushikilia msimamo wao wa kutoondoka eneo hilo na kuahidi kuoambana nao vikali watakapoingia leo.

“Sisi hatupingani na sheria bali tunaiachia mahakama itoe maamuzi yake kisheria lakini kwa sasa hatutaondoka hadi mahakama itakapotoa maamuzi” alikaririwa akisema, Bw. Hariri.

Bw. Hariri alieleza kuwa hadi sasa hawajakubali kusaini mkataba wa viwanja walivyopewa Chanika kwa madai kuwa wana wasiwasi na navyo kwani watakaposaini mkataba huo, watakuwa wamejiondoa wenyewe katika eneo hilo.

Alimshukuru Rais Jakaya Kikwete pamoja na tume iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa, Bw. Kandoro kwa kushughulikia suala lao na kuhakikasha wamepata haki yao ya msingi.


 


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents