Mombasa hali ya chakula mbaya – Mashuhuda

Gharama za bidhaa mjini Mombasa hasa vyakula zimepanda mara dufu kutokana na maduka kutofunguliwa.

Na Dunstan Bahai, Horohoro



Gharama za bidhaa mjini Mombasa hasa vyakula zimepanda mara dufu kutokana na maduka kutofunguliwa.


Hali hiyo imechangiwa na wafanyabiashara kutoka Tanzania kupitia mpaka wa Horohoro kusita kupeleka bidhaa zao wakihofia machafuko ya kisiasa yanayoendelea.


Nipashe ilishuhudia malori madogo aina ya Fuso yaliyosheheni mananasi na viazi yakiwa mpakani hapo kusubiri kuingia Mombasa.


Baadhi ya wananchi wanaosafiri kwa mabasi kupitia mpaka huo, walinunua vyakula vya kila aina, matunda na mbogamboga kupeleka mjini Mombasa.


Mwanamke mmoja kutoka Mombasa aliyekuwa Tanga kwa ajili ya harusi aliyejitambulisha kwa jina la mama Fadhila, alisema aliondoka huko Desemba 28 baada ya kupiga kura.


Alisema pamoja na familia yake walikwenda mkoani Tanga kwenye harusi, kabla hawajarejea wakasikia machafuko, hali ambayo imewafanya wasite kurudi.


“Baba watoto wangu kaniambia nirudi Mombasa ndiyo tunaelekea huko vitu vimepanda bei na havipatikani, unaona mwenyewe kwenye basi humu mifuko yote hii ni unga, mchele, sukari na vitu vingine, hali ni mbaya kwakweli,“ alisema.


Baadhi ya wachuuzi waliokutwa mpakani Horohoro walisema wanasafirisha vyakula kwenda kuuza Mombasa kwani bidhaa hizo hakuna.


Raia mmoja wa Kenya, Paragu Ali, alisema mfuko wa unga wa super sembe wa kilo 25 unanunuliwa mkoani Tanga kwa Sh. 900 za Kenya, karibu sawa na Sh.17,000 za Tanzania na Mombasa huuza kwa Sh. 20,000 za Tanzania.


Kwa upande wa sukari, alisema kilo 50 hununuliwa kwa Sh. 3,300 za Kenya.


Naye Bi. Khadija Hariri, ambaye mwishoni mwa wiki alifanikiwa kuingia Tanga kutoka Mombasa akiwa na wajukuu na mtoto, alisema mafuta ya taa ni adimu kipindi hiki.


Alisema mkate mkubwa uliokuwa ukiuzwa Sh. 40 za Kenya, umefikia Sh.50 sasa.


“Unajua kama upo Kenya huwezi jua mateso wanayopata Wakenya, hali ni mbaya , tunaomba haya masuala ya kisiasa yatafutiwe ufumbuzi,“ alisema.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents