Habari

Moto waua mume, mke Dar

Watu wawili mume na mke wamekufa jana alfajiri baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi maeneo ya Magomeni Kota, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, kuteketea kwa moto.

Na Mwajabu Mleche

 
Watu wawili mume na mke wamekufa jana alfajiri baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi maeneo ya Magomeni Kota, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, kuteketea kwa moto.

 

Waliokufa katika ajali hiyo iliyotokea nyumba Na. 227 ni Othman Magola (32), na mkewe Aneth Robert (29), ambao hawakuwa na watoto.

 

Miili yao ilikutwa ikiwa imeng`ang`ania dirishani, kitendo kinachoonyesha walikuwa wakijaribu kuokoa maisha yao kwa kupita dirishani bila mafanikio.

 

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Bw. Jamal Rwambow, alithibitisha kutokea kwa ajili hiyo.

 

Kaka wa marehemu Aneth, Bw. George Robert ambaye ni mkazi wa Mbezi ameliambia Nipashe katika eneo la tukio jana asubuhi kwamba alipata habari za ajali hiyo alfajiri hiyo akiwa njiani kwenye shughuli zake.

 

`Nikiwa katika maeneo ya Magomeni, mtu mmoja alinifahamisha kwamba kuna ajali ya moto inayoendelea maeneo ya Magomeni Kota, jambo ambalo lilinifanya niteremke kwenye gari na kwenda kufuatilia ajali hiyo,` alisema Bw. Robert.

 

Alisema wakati anakaribio nyumba iliyokuwa inaungua aligundua kwamba ni ile anayoishi dada yake na shemeji yake.

 

Bw. Robert alisema kwamba alipofika kwenye eneo la ajali alikuta gari la zimamoto na wafanyakazi wake wakiwa wameduwaa huku wananchi waliokuwepo wakijitahidi kuuzima moto huo.

 

Mtu mwingine aliyeshuhudia ajali hiyo, Bw. Aziz Fundi, mkazi wa nyumba Na. 228 ambayo pia imeungua, alisema kwamba moto huo ulianza majira ya saa 10.00 alfajiri na uliendelea hadi saa 12.00 asubuhi.

 

`Majira ya saa 10.00 usiku nilisikia kelele zikiniamsha kutoka ndani kwamba kulikuwa na moto,` alisema Bw. Fundi.

 

Alieleza kwamba mara baada ya kuamka walipiga simu Kikosi cha Zimamoto saa 10.00 alfajiri lakini gari hilo lilifika saa 12.00 asubuhi na kushindwa kabisa kufanya shughuli za uokoaji kama ilivyotarajiwa.

 

Alisema kwamba wananchi wenyewe ndio waliofanikiwa kuzima moto huo na kubomoa milango ili kutoa miili ya watu hao wawili ambayo iliungua kiasi cha kutoweza kutambulika.

 

`Hali ya miili yao ilikuwa inatisha kwa jinsi ilivyokuwa imeungua vibaya kwa moto� Pamoja na polisi kufika saa 11.45 asubuhi, miili hiyo ilibaki kwa kipindi kirefu baada ya gari hilo la Kituo cha Polisi Magomeni kuondoka eneo la ajali ili kwenda kufanya kazi nyingine,` alisema.

 

Alisema kwamba wakati wananchi walipokuwa wakifanya taratibu za kukodi gari ili kuondoa maiti hizo ndipo lilipofika gari la polisi lililozichukua na kuzipeleka katika hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya kuhifadhiwa.

 

Hadi sasa chanzo cha moto huo hakijafahamika ingawa baadhi ya majirani katika eneo la tukio wanasema ni hitilafu ya umeme ambao ulikatika tangu saa 8:00 usiku na kurejea saa 10.00 alfajiri.

 

Halikadhalika, haikuweza kufahamika kiasi cha hasara ambazo zimepatikana kutokana na kuteketea kabisa kwa nyumba hizo mbili.

 

Katika tukio lingine lililotokea mwishoni mwa wiki, huko Wazo Hill, eneo la Msikitini, gari lisilofahamika lilipita kwa kasi na upepo wake kumsomba mtu anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 20 na 25 ambaye hakufahamika jina na kudondoka na kufariki dunia.

 

Kamanda Rwambow alisema, mtu huyo alikuwa akiendesha baiskeli iliyopakia majani ya ng`ombe.

 

Aidha, katika tukio lingine watu 11 wamejeruhiwa baada ya magari kugongana eneo la Kimara Baruti.

 

Kamanda Rwambow alisema, basi lenye namba za usajili T 514 AKQ aina ya Scania lililokuwa likitokea Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo kuelekea Kyela, Mbeya, liligongana na gari namba T 464 AGJ Toyota Canter lililokuwa likitokea barabara ndogo ya Ubungo kuelekea barabara kubwa.

 

Aliwataja madereva waliosababisha ajali hiyo kuwa ni dereva wa basi, Esaya Maneno (36), mkazi wa Tukuyu, Mbeya na Boniface Mwalinde (35), mkazi wa Mbeya.

 

Kamanda alisema, katika ajari hiyo, watu 11 walijeruhiwa, ambapo abiri saba walitibiwa na kuruhusiwa na wanne walilazwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili.

 

Waliolazwa wametajwa kuwa ni Tekra Ngulunde, mtoto mwemye umri miezi miwili, Cosmas Ngulunde miezi minne, Joyce Mgau (66) na dereva wa basi Mwalinde.

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents