Habari

Mpango wa Uingereza kujitoa umoja wa Ulaya wakumbwa na jinamizi, Bi. Theresa May aomba tarehe ya kujitoa isogezwe mbele

Mpango wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Bi. Theresa May wa kuhusu Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya (EU), maarufu kama Brexit umepatwa na pigo lingine lililosababisha Waziri huyo kuomba tarehe ya taifa hilo kujitoa isogezwe mbele kutoka Machi 29 hadi Juni 30 mwaka huu.

Related image
Theresa May

Hali hiyo imekuja baada ya Spika wa Bunge la nchi hiyo, John Bercow kutangaza kuwa mpango huo hauwezi kupigiwa tena kura bungeni, mpaka utakapofanyiwa marekebisho makubwa tofauti na yale ya kwanza.

Katika tangazo la kushtukiza juzi jioni, Spika Bercow alisema wabunge hawawezi kuupigia kura mpango ule ule walioukataa awali katika msimu mmoja wa Bunge.

Akitumia kigezo cha mwaka 1604, Spika Bercow alisema itakuwa kinyume cha sheria kwa Serikali kuwasilisha tena mpango uliokwishapingwa awali na wabunge.

Tangazo hilo la Spika Bercow limekuja wakati Serikali ya May inahangaika kuwashawishi Wabunge kuukubali mpango huo wa Brexit, ambao tayari wamekwishaupiga chini mara mbili.

Bi. Theresa May alitaka Bunge nchini humo kupiga kura kwa mara nyingine tena kabla ya Machi 29, tarehe ambayo Umoja wa Ulaya iliitaka Uingereza kufikia siku hiyo iwe tayari imejitoa.

Spika Bercow alitoa ufafanuzi kuhusu tangazo lake, akisema hataki lichukuliwe kama kauli ya mwisho kuhusu Brexit, bali kama sharti ambalo Serikali inapaswa kulitimiza, ili yeye aweze kuandaa kura ya tatu bungeni kuamua juu ya mpango huo.

Kwa upande mwingine, Waziri wa Brexit, Steve Barclay akijibu tangazo la Spika Bercow alisema hiyo inamaanisha hakutakuwa na upigaji kura leo na hivyo Uingereza itachelewa kidogo kuondoka EU.

Bi. May alitazamia kuwa mpango wake wa Brexit ungeshinda safari hii iwapo ungepigiwa kura hii leo, lakini kufuatia maamuzi ya Spika wa Bunge imemlazimu kuuomba Umoja wa Ulaya kusogeza mbele tarehe ya taifa hilo kuondoka rasmi EU hadi Juni 30.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents