Siasa

Mrema alia na mawaziri

MWENYEKITI wa Taifa wa Tanzania Labour, Bw. Augustino Mrema amemshauri Rais Jakaya Kikwete kulivunja Baraza lake la Mawaziri ili kupata mawaziri watakaochapa kazi na kuepusha upinzani mkali kwenye uchaguzi mkuu ujao 2010 kama ule uliomkabili Rais Mwai Kibaki wa Kenya na kupoteza mawaziri wengi kwenye uchaguzi uliomalizika jana nchini humo.

Francis Godwin na Yohanes Mbelege, Moshi

 

MWENYEKITI wa Taifa wa Tanzania Labour, Bw. Augustino Mrema amemshauri Rais Jakaya Kikwete kulivunja Baraza lake la Mawaziri ili kupata mawaziri watakaochapa kazi na kuepusha upinzani mkali kwenye uchaguzi mkuu ujao 2010 kama ule uliomkabili Rais Mwai Kibaki wa Kenya na kupoteza mawaziri wengi kwenye uchaguzi uliomalizika jana nchini humo.

 

Bw. Mrema alitoa kauli hiyo mjini hapa jana wakati akitoa maoni ya chama chake kwa waandishi kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Kenya.

 

Alisema binafsi muda wote alikuwa akifuatilia mwenendo wa uchaguzi huo na kuamua kurejea mkoani Kilimanjaro ili aweze kujumuika na wananchi wa Kenya wanaoishi mkoani humo, kusherekea kudondoshwa mawaziri wengi wa Serikali tawala ambao ni dhahiri inaonesha walishindwa kutekeleza wajibu wao.

 

“Kweli ndugu zangu waandishi moja ya mambo yanayonifanya nifurahi zaidi …ni pamoja na matokeo ya uchaguzi kwa upande wa mawaziri wa Kenya…Kweli nasema mawaziri wazembe watambue kuwa Watanzania sio mandondocha… miaka mitatu si mingi wajiandae kunyolewa na wembe ule ule unaotumika Kenya,” alisema.

 

Bw. Mrema alisema kuwa binafsi anapongeza kazi nzuri iliyofanywa na Rais wa Kenya ,Bw. Mwai Kibaki lakini kutowajibika ipasavyo kwa mawaziri kumesababisha kunyimwa kura na wananchi.

 

Akifafanua kuhusu Baraza la Mawaziri la Tanzania, Bw Mrema alisema baadhi yao ni wababaishaji na wasio na uwezo jambo linalomfanya Rais Kikwete kushindwa kutekeleza ahadi zake kwa wananchi waliomchagua.

 

Bw. Mrema alimshauri Rais Kikwete kutangaza matokeo ya tume mbalimbali anazoziunda hadharani ili kuongeza imani kwa wananchi.

 

Aidha ameshauri kuvunjwa Baraza la Mawaziri haraka iwezekanavyo ili kuinusuru CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, vinginevyo mawaziri hao wataiponza CCM na kunyimwa kura na wananchi.

 

Bw. Mrema pia amewataka wananchi kujifunza kutoka Kenya na kukubali kufanya mabadiliko katika masuala ya siasa kwani mambo hayo si misahafu na mabadiliko mara nyingi huleta maendeleo.

 

Bw. Mrema alisema matokeo ya uchaguzi wa Kenya ni sehemu ya semina kwa wapinzania kujiandaa na uchaguzi wa mkuu ujao.

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents