Habari

Msafara wa kiongozi wa Korea Kim Jong Un, watikisa China, yuko China kwa ajili ya mazungumzo na Xi Jinping (+ Video)

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amewasili kwenye mji mkuu wa China kwa ziara ya siku nne, Beijing baada ya kualikwa na Rais wa nchi hiyo, Xi Jinping.

Shirika la habari la Korea Kaskazini, KCNA limeripoti kuwa Kim aliyeondoka jana mchana kwa kutumia treni maalum, ameongozana na mkewe, Ri Soil Ju pamoja na mpatanishi mkuu katika mazungumzo ya nyuklia, Kim Yong Chol, Waziri wa Mambo ya Nje, Ri Yong Ho na Waziri wa Ulinzi, No Kwang Chol. Kim atakutana na Rais Xi Jinping kwa mara ya nne chini ya kipindi cha mwaka mmoja.


Kwa mujibu wa DW, Baada ya kuwasili Kim alisindikizwa chini ya ulinzi mkali wa polisi kuelekea kwenye nyumba ya wageni katika Ikulu ya China. Kiongozi huyo wa Korea Kaskazini ameianza ziara hiyo leo ikiwa ni kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa, ambapo anatimiza umri wa miaka 35.

Ziara hiyo inafanyika huku maandalizi ya mkutano wa kilele kati ya Kim na Rais wa Marekani Donald Trump yakiendelea. Imeripotiwa kuwa maafisa wa Marekani na Korea Kaskazini wamekutana Vietnam kujadiliana kuhusu eneo utakapofanyika mkutano wa kilele kati ya Kim na Trump.

Kim na Jinping walikutana kwa mara ya kwanza mwezi Machi mwaka uliopita, miaka sita baada ya Kim kumrithi baba yake kuiongoza Korea Kaskazini. Uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili ulirejea katika hali ya kawaida mwaka uliopita, baada ya kuwa mbaya kutokana na majaribio ya makombora ya nyuklia ya Korea Kaskazini ambayo yalikuwa yanatishia kuanzisha vita na Marekani.

Msemaji wa serikali ya Japan, Yoshihide Suga amesema wanaifatilia kwa umakini ziara ya Kim nchini China. ”Tunaifatilia kwa karibu ziara hii na kwa maslahi makubwa. Tunafanya taratibu za kupata taarifa na kuzifanyia uchambuzi. Tunatarajia China itatuarifu zaidi kuhusu ziara hii,” alisema Suga. Hata hivyo, Suga amekataa kuzungumzia kile kinachotarajiwa katika mkutano wa Kim na Jinping.

China ni mshirika muhimu wa kidiplomasia na kibiashara wa Korea Kaskazini na ziara hii inaashiria kwamba nchi hizo mbili jirani zinaratibu sera kabla ya mazungumzo ya Trump na Kim kuhusu kupunguza matumizi ya silaha za nyuklia katika Rasi ya Korea

Hata hivyo, katika hotuba yake ya salamu za Mwaka Mpya Kim alionya kwamba Korea Kaskazini huenda ikabadili mwelekeo wake kuhusu mazungumzo ya nyuklia, iwapo Marekani itaendeleza vikwazo vyake.

Kim anatarajiwa pia kuizuru Korea Kusini kwa mara ya kwanza baadae mwaka huu. Shirika la habari la Korea Kusini, Yonhap limesema nchi hiyo imeisifu ziara ya Kim nchini China na imeelezea matumaini yake huenda ikasaidia kupunguza matumizi ya silaha za nyuklia na kuleta amani katika Rasi ya Korea.

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents