Burudani

Msanii wa Jagwa Music, Jack Simela na wenzake watano wazikwa Morogoro

Mmoja kati ya wasanii wa kundi la Jagwa Music, Jackson Kazimoto maarufu Jack Simela amezikwa jana Desemba 10, katika makaburi ya Bigwa mkoani Morogoro.

Jack amezikwa katika makaburi hayo pamoja na mjomba wake, Ibrahim Karata ambaye ni mtoto wa shangazi yake, Elizabeth Kazimoto aliyezikwa jana katika makaburini hapo.

Baba wa msanii huyo, Leonard Kazimoto aliambia Mtanzania Digital kuwa msanii huyo, mjomba wake na wenzake watano walifariki dunia wakiwa njiani kwenda makaburi ya bigwa kwajili ya mazishi ya shangazi wa msanii huyo.

“Wakati tunaenda kuzika tulitoka wote hapa maana msiba ulikuwa Mwembesongo wao walikuwa saba wote waliingia kwenye gari lao dogo walipitia barabara kuu ya Moro/ Dar sisi tulipita barabara ya zamani ya Dar, tulipofika makaburini ilituchukua muda kuwasubiri maana tulitaka Jack amzike shangazi yake na pia Ibrahimu Karata naye amzike mama yake ila tulipoona hawatokei tukazika.

“Kumbe walikuwa wamepata ajali eneo la nane nane maarufu kwa jina la Jordan na wote sita wamefariki dunia isipokuwa mmoja amelazwa yupo hoi hospitalini,’’ amesema.

Amesema waliporudi nyumbani walishangaa kuona vilio vikizidi walipohoji ndipo wakaambiwa kuna msiba mwingine Jack, Ibrahim na wenzao wengine waliokuwa kwenye gari ndogo waligongana na gari kubwa.

Naye shangazi wa msanii huyo, Yasinta Kazimoto amesema alimlea msanii huyo aliyezaliwa 1986 tangu alipokuwa na miaka nane baada ya mama yake mzazi kufariki mwaka 1994.

“Nilimlea vizuri hadi mwaka 2004, alipokuja kuchukuliwa na meneja wake, Gola tangu alipomuona alipokuwa akiimba kwenye moja ya maonyesho ya Jagwa Manzese mkoani hapa hadi sasa mauti yemamkuta ameishi katika kundi la Jagwa kwa miaka 13, alikuwa mtu safi alinipa zawadi kila aliposafiri sikupata naye tabu katika malezi yake,’’ amesema Shangazi yake.

Ameongeza kwamba msanii huyo ameacha watoto watatu, Saidi (18), Nuru (17) na Leonard (4).

Meneja wa mwanamuziki huyo, Abdallah Salehe maarufu meneja Gola amesema kifo cha msanii huyo aliyehitimu elimu ya msingi Shule ya Mwembesongo mkoani hapa ni pigo kubwa kwa tasnia ya muziki wa mchiriku na kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa amebaki kuubeba muziki huo.

“Jack ndiye alikuwa amebaki kuubeba muziki wa mchiriku kifo chake ni pigo kubwa kwa muziki huo, kwani uwezo na uvumilivu wake baada ya wasanii wengi kuliacha kundi la Jagwa ndiyo ulikuwa ukibeba kundi hilo kote ndani na nje ya nchi walipokuwa wakifanya maonyesho yao,’’ amesema Gola.

Hata hivyo baadhi ya wasanii ambao hawakutaka kutajwa majina yao walishangazwa na wadau wa muziki huo kutokufika katika mazishi ya msanii huyo huku wakiongeza kuwa wajenge utamaduni wa kuzikana, sababu wote njia yao ni moja.

Source: Mtanzania

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents