Habari

Mshitakiwa alikuwa kitandani bila shati…

Shahidi katika kesi ya kudai rushwa ya ngono inayomkabili Mkuu wa Shule, amedai kuwa, alimkuta mshtakiwa amekaa kitandani huku akiwa amevua shati na kubaki na fulana nyeupe na pembeni yake, aliketi binti ambaye hakumfahamu.

Na Claudia Kayombo, Pwani



Shahidi katika kesi ya kudai rushwa ya ngono inayomkabili Mkuu wa Shule, amedai kuwa, alimkuta mshtakiwa amekaa kitandani huku akiwa amevua shati na kubaki na fulana nyeupe na pembeni yake, aliketi binti ambaye hakumfahamu.


Shahidi huyo, Hamis Shomari (20) ambaye ni mhudumu wa nyumba ya kulala wageni ya Matumbi, iliyoko Tabata Matumbi, jijini Dar es Salaam, alikuwa akitoa ushahidi wake katika Mahakama ya Wilaya Kisarawe mbele ya Hakimu Mwandamizi Mfawidhi, Bw. Fundi Kaniki.


Mshtakiwa katika kesi hiyo ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Janguo, Edward Tindikali (48), ambapo anadaiwa kumuomba mwanafunzi wake wa kidato cha pili rushwa ya ngono kwa ahadi ya kumwezesha afaulu mitihani yake.


Akiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) mkoani Pwani, Bi. Thuwaiba Husein, shahidi huyo alidai kuwa, siku ya tukio, mshtakiwa alikwenda kukodi chumba katika nyumba hiyo.


Shahidi huyo alidai kuwa, mshtakiwa huyo alikodishwa chumba namba 16 katika nyumba hiyo ya kulala wageni.


Aliongeza kuwa baada ya kumpa funguo za chumba, aliendelea na shughuli zake hadi baadaye aliposikia kelele kutoka katika chumba hicho.


Alidai kuwa, alilazimika kwenda na ndipo alipomkuta mshtakiwa akiwa amevua shati na kubakiwa na fulana nyeupe huku pembeni yake akiwa ameketi binti mmoja ambaye hakumtambua.


Naye shahidi wa tano katika katika kesi hiyo ambaye ni mjumbe wa shina namba 21 eneo la Tabata Matumbi, alidai kwamba, siku ya tukio, akiwa nyumbani kwake, alifuatwa na watu waliojitambulisha kuwa ni maofisa wa TAKURU.


Alidai kuwa, maofisa hao wa TAKURU walimweleza kuwa, kuna tukio la Mwalimu kukamatwa akiwa katika harakati za kutaka kufanya ngono na mwanafunzi wake katika nyumba ya kulala wageni iliyoko eneo lake.


Mjumbe huyo, Bw. Issa Ramadhani, alidai kuwa, alikwenda eneo la tukio ambapo alimkuta mshtakiwa akiwa amekaa kitandani huku akiwa amevua shati na kubaki na fulana nyeupe na pembeni yake alikuwapo amekaa binti.


Shahidi huyo alidai kuwa, maofisa wa TAKURU walimwambia walimfahamu mshtakiwa kutokana na kuwekewa mtego.


Alidai kuwa, walipomhoji mshtakiwa, alijieleza kwamba ni mkazi wa Msanga, wilayani Kisarawe na ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Janguo.


Shahidi huyo aliongeza kuwa, alipomwuliza binti aliyekuwa ameketi kitandani, alidai kuwa, ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule hiyo.


Binti huyo alidai kuwa, alifika katika nyumba hiyo ya kulala wageni baada ya mwalimu huyo kumrubuni kuwa, iwapo atafanya naye mapenzi, atampasisha mitihani yake ya kidato cha pili ambayo alishindwa mwaka 2005.


Naye Mkuu wa TAKURU wilayani Kisarawe, Bw. Cassian Mhepangwa (33), alidai kuwa, Septemba 25, mwaka jana, majira ya asubuhi, binti mwenye umri wa miaka 17 (jina limehifadhiwa), alikwenda katika ofisi yake kutoa malalamiko ya kuombwa rushwa ya ngono na Mkuu huyo wa Shule.


Shahidi huyo alidai kuwa, binti huyo alimwambia kuwa, amekuwa akisumbuliwa kwa muda mrefu na mkuu huyo wa shule akitaka ampe ngono ili aweze kufaulu mitihani yake ya kidato cha pili.


Bw. Mhepangwa aliongeza kuwa, binti huyo alimwambia kwamba, kwa kuwa mshtakiwa ni Mkuu wake wa Shule, anashindwa cha kufanya ili aweze kusalimika kutokana na kero anazozipata kutoka kwake.


Alidai kuwa, baada ya kusiliza malalamiko ya binti huyo, alimpa mbinu za kumkubalia mshtakiwa ili siku atakayotaka kufanya naye ngono, atoe taarifa katika ofisi yake nao watamtia mbaroni.


Alidai kuwa, Oktoba 18, mwaka jana, binti huyo alimpigia simu kumjulisha kuwa, amemkubalia mwalimu huyo na kwamba amemwambia siku inayofuata, yaani Novemba 19, mwaka jana, waende jijini Dar es Salaam mwalimu huyo akatimize azma yake.


Shahidi huyo alidai kuwa, baada ya taarifa hizo, aliwapa kazi maofisa wake wadogo wawili ya kuwasiliana na binti huyo kila hatua, hadi mshtakiwa alipofikia ambapo ilibainika kuwa, alikodi nyumba ya kulala wageni ya Matumbi na hivyo kufanikiwa kumnasa akiwa katika harakati za kutaka kumwingilia kimwili binti huyo.


Kesi hiyo itaendelea tena Aprili 30, mwaka huu ambapo mashahidi wengine watatu wa upande wa mashtaka wanatarajiwa kutoa ushahidi wao na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents