Msichana ombaomba mbaroni kwa kuiba mtoto

Polisi mkoani Dodoma, inamshikilia mtoto mwenye umri wa miaka 12 (jina limehifadhiwa) kwa tuhuma za kumuiba mtoto wa kiume mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.

Na Theodos Mgomba, PST Dodoma



Polisi mkoani Dodoma, inamshikilia mtoto mwenye umri wa miaka 12 (jina limehifadhiwa) kwa tuhuma za kumuiba mtoto wa kiume mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.


Mtuhumiwa huyo anadaiwa kumuiba mtoto huyo kutoka jijini Dar es Salaam ili akamtoe zawadi kwa wazazi wake walioko jijini Mwanza.


Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Bw. Michael Kamuhanda alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 4:00 asubuhi.


Kamanda Kamuhanda alisema siku hiyo ya tukio, wasamaria wema walimkuta mtoto huyo akiwa amebeba mtoto huku akirandaranda mitaani kuomba msaada.


Alisema baada ya kumkuta hivyo, walimhoji alikotoka na ndipo aliposema kuwa alitokea jijini Dar es Salaam.


Alifafanua kuwa, baada ya kupata jibu hilo, waliamua kumpeleka kituo kikuu cha polisi mjini hapa kwa mahojiano zaidi.


Kamanda Kamuhanda alisema baada ya kuhojiwa binti huyo alikiri kuwa yeye ni ombaomba aliyekuwa akiishi jijini Dar es Salaam na alimuiba mtoto huyo eneo la Magomeni Mapipa kwa nia ya kumpeleka kama zawadi kwa wazazi wake wanaoishi jijini Mwanza.


Alisema binti huyo alisema aliweza kumuiba mtoto huyo baada ya kumkuta akiwa katika moja ya nyumba ambayo huonyesha picha za video kwa watoto.


Kaimu Kamanda huyo alisema binti huyo alieleza kuwa, alimuiba mtoto huyo Machi 23, mwaka huu ili ampeleke katika kijiji cha Nyakamongo mkoani Mwanza lakini alipofika mkoani hapa, aliishiwa nauli.


Alisema baada ya kuishiwa nauli, aliamua kuomba toka kwa wasamaria wema ili aweze kupata fedha kwa ajili ya nauli hiyo ikiwa ni pamoja na kumhudumia mtoto aliyemuiba.


Alisema Jeshi la Polisi limefanya utaratibu wa kumsafirisha mtoto huyo kwenda jijini Dar es Salaam chini ya ulinzi wa polisi ili aweze kuonyesha mahali alikomuiba mtoto huyo.


 


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents