Habari

Mtandao waiba mabilioni

MTANDAO mpya wa wizi wa fedha za serikali zilizotengwa kwa ajili ya malipo ya mafao ya waliokuwa wafanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, umeibuka.

na Martin Malera


MTANDAO mpya wa wizi wa fedha za serikali zilizotengwa kwa ajili ya malipo ya mafao ya waliokuwa wafanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, umeibuka.


Tayari mtandao huo umeishaiba mamilioni ya fedha za wafanyakazi wa jumuiya hiyo kwa kutumia nyaraka feki na kuwaacha wahusika halisi wakiendelea kusaga miguu kufuatilia malipo yao bila mafanikio.


Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima kwa wiki kadhaa sasa, kuanzia jijini Dar es Salaam na baadaye Dodoma kunakoendelea kikao cha Bunge, umebaini kuwa mtandao huo umejizungushia katika idara tatu nyeti za serikali na kundi la wajanja wachache la vijana wa mitaani. Idara hizo ni pamoja na Kitengo cha Vizazi na Vifo, Mahakama na Hazina.


Mtandao huo pia unahusisha ofisi za mashirika yaliyokuwa chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na mtandao wa mataalam wa kuchonga nyaraka na mihuri feki ulioshamiri mitaani.


Uchunguzi wetu wa kina na wa uhakika, umebaini kuwa baadhi ya maofisa katika idara hizo za serikali, wamekuwa wakishirikiana na kikundi cha wajanja wa mitaani kutengeneza nyaraka feki kwa kutumia majina feki na hatimaye kupata mamilioni hayo kirahisi.


Hali hiyo imekuwa ikiwaacha wahusika wakiendelea kusota na kuilaumu serikali kwamba inawazungusha kupata malipo yao.


Kwa mujibu wa uchuguzi wetu, nyaraka nyingi feki, hasa za kuthibitisha mtu fulani alikuwa mfanyakazi wa jumuiya hiyo kutoka katika moja ya mashirika yaliyokuwa chini ya Jumuiya ya Afrika Mashairki, huchongwa mitaani kitaalam kwa kutumia mtandao wa kutengeneza nyaraka feki, vikiwemo vyeti vingi vya shule, vyuo vikuu, pasipoti na hata vyeti vya vyuo vikuu vya nje ambavyo Tanzania Daima imevipata.


Fedha zinazoibwa kirahisi kupitia mtandao huo wa wizi ni zile zinazotokana na mirathi. Vyeti vya mirathi ya wanamtandao huo wa wizi vinadaiwa kutolewa na kitengo cha Vizazi na Vifo baadaye nyaraka hizo pamoja na zile feki za kutoka kwenye Mashirika yaliyokuwa chini ya Jumuiya hiyo, hufikishwa Hazina kwa ajili ya hatua zingine za kufuatilia malipo ya mafao ya watumishi wa jumuiya hiyo.


“We huoni vijana hapa kijiweni walivyobadilika, wengi wanabadilisha magari kama nguo, cheni za gold za nguvu, hawana kazi. Kazi yao ni kuja kijiweni hapa na kupanga mikakati ya kuiba fedha hizo.


“Angalia vijana walioko pale Vizazi na Vifo, mishahara midogo, lakini kila mtu ana gari. Hebu jiulize wamepataje? Waandishi wa habari fichueni hayo. Wenye mirathi wanateseka, wajanja wa mtaaani wanatanua,” kilisema chanzo chetu cha habari na kutoa orodha ya baadhi ya vijana na maofisa wa idara hizo wanaodaiwa kuwamo kwenye mtandao huo.


Wiki iliyopita, Waziri wa Fedha, Zakia Meghji wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake, alizungumzia suala la wizi wa mtandao huo.


Alisema wizara yake hadi sasa imebaini kuwapo maombi feki 182 kati ya mengi yaliyowasilishwa wizarani hapo.


Kutokana na udanganyifu huo, alisema zoezi la malipo kwa ajili ya wafanyakazi hao linafanywa kwa makini, ili kuhakikisha kuwa haki inatendeka na kuhakikisha kuwa malipo hayo yanafanyika kwa watu wanaostahili tu.


Alisema kabla ya malipo, wizara hufanya uchunguzi kubaini maombi yapi ni halali na yapi si halali, ili wale wanaostahili walipwe na wale wadanganyifu wasilipwe na ikiwezekana wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.


“Hadi sasa, madai 182 yamebainika kuwa ni maombi yenye udanganyifu. Wizara bado inaendelea kupokea nyaraka za uthibitisho wa madai ya malipo kutoka katika mashirika yaliyokuwa chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Meghji.


Kwa mujibu wa habari hizo, mtandao huo una mbinu ya kubaini madai yenye malipo ya kiwango cha juu na baada ya hapo, huingia mitaani kutafuta nyaraka na vielelezo feki, ili kuthibitisha kuwa wao ni wasimamizi wa mirathi na hatimaye kupata pesa hizo.


Katika harakati za kufuatilia malipo hayo, baadhi ya wasimamizi wa mirathi waliwahi kuripotiwa kuwa, majina yao hayamo katika orodha ya watu wa mirathi wanaodai malipo yao, na kwamba wamefuatilia bila mafanikio na wengine kukata tamaa.


Kwa mujibu wa Waziri Meghji hadi kufikia Juni 30, mwaka huu, wastaafu 36,455 wamekwishalipwa na kiasi cha fedha kilichotumika kuwalipa ni sh bilioni 116.4.


Alisema kati ya hizo, sh bilioni 31.463 zimelipwa kama mirathi kupitia mahakama mbalimbali nchini.


Serikali ilianza kutoa malipo ya mafao ya wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki Septemba mwaka 2005.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents