Michezo

Mtanzania aibuka kidedea kwenye Marathon India

Mtanzania Alphonce Simbu, amefanikiwa kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania kwenye mbio ndefu za Mumbai Marathon ya mwaka huu huku akiwapiku Mkenya Joshua Kipkorir pamoja na wakimbiaji wengine wazoefu kutoka mabara mbalimbali.

Alphonce Simbu

Mashindano hayo yajulikanayo kama Standard Chartered Mumbai Marathon hufanyika Jumapili ya tatu ya mwezi Januari katika jiji la Mumbai nchini India na yanaaminika kuwa ni mbio kubwa kabisa barani Asia kwa idadi ya washiriki wanaomaliza mbio.

Mwanariadha huyo ambaye yupo chini ya udhamini wa kampuni ya Multichoice Tanzania, aliibuka mshindi baada ya kutumia muda wa saa 2:09:28 muda ambao ni mzuri kwa mbio za aina hiyo.

Simbu amesema kuwa anaamini ushindi huo umesababishwa na maandalizi aliyoyafanya.

Amesema ushindi huo kwake ni changamoto kwa mashindano mengine makubwa na kwamba huo ni mwanzo tu. Amesema ushindi huo siyo wake peke yake au wathamini wake , bali ni ushindi wa Taifa zima la Tanzania.

Kwa upande wa Serikali, Waziri wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo, Mh. Nape Nnauye amempongeza kupitia kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akisema , “Tumefanikiwa tena, hongera Simbu, hongera RT (Chama cha Riadha Tanzania), asanteni Multichoice Tanzania kwa kumsapoti. Mungu ibariki Tanzania.”

Mkuu wa Mahusiano wa Multichoice Tanzania Johnson Mshana amesema Multichoice imefurahi sana kwa matokeo huku akisisitiza kuendelea kumdhamini Simbu kwa mujibu wa makubaliano yao, ili kuhakikisha anaendelea kufanya vyema na kuliletea taifa sifa kubwa.

“Tulichukua jukumu la kumdhamini Simbu katika mazoezi na maandalizi yake kwa kipindi cha mwaka mzima, kwani tunafahamu fika kuwa mazoezi na maandalizi ndiyo siri kubwa ya mafanikio katika mchezo wowote.

Alisema Mshana na kuongeza “Dhamira yetu kubwa ni kuinua vipaji na kulirejesha taifa letu kwenye ramani ya dunia katika ulingo wa michezo na burudani”

Alphonce anatarajiwa kurejea Tanzania Jumatatu hii.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents