Habari

Mtanzania alalamikia askari Zimbabwe

MFANYABIASHARA Mtanzania anayefanya shughuli zake nchini Zimbabwe, amewataka Watanzania kushinikiza mabadiliko katika nchi hiyo ambayo hali ya mambo ni mbaya sana.

na Tamali Vullu


MFANYABIASHARA Mtanzania anayefanya shughuli zake nchini Zimbabwe, amewataka Watanzania kushinikiza mabadiliko katika nchi hiyo ambayo hali ya mambo ni mbaya sana.



Akizungumza na Tanzania Daima mwishoni mwa wiki, mfanyabiashara huyo alisema hali hiyo imefikia hatua ya kuwafanya hata watu wasio Wazimbabwe kupatwa na matatizo mengi wakati wakiwa nchini humo.



Mfanyanbiashara huyo, Wande John, alisema hivi sasa askari wa Zimbabwe, mbali ya kuwanyanyasa watu wa nchi hiyo, wamekuwa wakiwatesa Watanzania na watu wengine kutoka nje ya nchi hiyo.



John alisema kuwa, mambo yaliyomtokea yeye binafsi, na yale aliyoyashuhudia yakiwatokea watu wengine, sasa yameanza kuthibitisha kuwa, nchi za Kiafrika zinatakiwa kuingilia kati masuala ya Zimbabwe kwa nia ya kutafuta suluhisho haraka iwezekanavyo.



Alisema Afrika inatakiwa kuingilia Zimbabwe na kuleta suluhu haraka kwa sababu yanayotokea huko hayawaathiri Wazimbabwe peke yao kama wengi wanavyodhani, bali huwaathiri hata wageni ambao hutembelea au hufanya kazi katika nchi hiyo.



Alidai kuwa, moja ya vitendo vya udhalilishaji wafanyabiashara wanaoingia nchini humo, ni kuvuliwa nguo na askari (ambao huko huitwa Kapokora), katika kile kinachodaiwa na askari hao kuwa ni upekuzi.



Aidha, askari hao huingiza dhuluma kwani mara nyingi wamekuwa wakiwanyang’anya wafanyabiashara bidhaa zao kwa madai ya kuwa wamekamata magendo.



Akizungumza kwa uchungu katika ofisi za gazeti hili mwishoni mwa wiki, John alidai kuwa, mwaka juzi kuna Mtanzania ambaye aliamua kujinyonga baada ya kufanyiwa unyama huo na askari wa Zimbabwe na kunyang’anywa fedha zote alizokuwa nazo.



John alisema hali ya Zimbabwe kwa sasa ni mbaya na wafanyabishara wanaofanya kazi nchini humo wanahitaji msaada wa haraka, ili kuondokana na hali hiyo ambayo imegharimu maisha ya wengi.



“Zimbabwe kuna vita ya maisha na wanaoumia zaidi ni wanawake, kwani wanaume wanakimbilia Afrika Kusini, Malawi na Botswana na kutelekeza familia zao,” alisema.



Mfanyabiashara huyo alisema kutokana na hali hiyo, kauli iliyopata kutolewa na Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo, kuwa matatizo ya Zimbabwe wanapaswa kuachiwa wananchi wa nchi hiyo, si sahihi hata kidogo.



“Kama askofu (Pengo) nilitegemea angetoa tamko la kutaka kuwanusuru Wazimbabwe, ambao miongoni mwao wapo Wakatoliki wengi. Pamoja na matatizo ya kisiasa, nchi hiyo haina chakula na hata kikipatikana ni kwa bei ya juu sana na hospitali hazina dawa,” alisema mfanyabiashara huyo mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam.



Pia alisema hakuna mawasiliano ya barabara kati ya kijiji na kijiji, hivyo, hali ya maisha katika maeneo hayo ni mbaya zaidi.



“…Hivi sasa kusafiri kutoka Zimbabwe mjini kwenda Bulawayo ni kama kwenda nchi jirani. Barabara hazifai kabisa. Morgan Tsvangirai ni kama kamsemo, lakini Zimbabwe kuna matatizo. Wazimbabwe wanampenda Profesa Anna Tibaijuka kwa kuwa alizungumza ukweli kuhusu hali ya Zimbabwe,” alisema.



Tibaijuka ni Mkurugenzi wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa. Mwaka jana alitoa kauli akilaani hatua ya Serikali ya Zimbabwe kubomoa kile kilichoitwa vibanda katikati ya mji wa Harare, kwa madai ya kuwahamisha watu waliokuwa wamevamia maeneo.



Mfanyabiashara huyo, alisema inasikitisha kuona kuwa Watanzania wengi hawaelewi uzito wa matatizo ya Wazimbabwe na akawataka wasichukulie matatizo hayo kirahisi, kwani watu wanaendelea kuumia na wengine kufa.



John alisema Zimbabwe inahitaji mabadiliko ya haraka na akasema hata Rais Robert Mugabe aking’oka sasa, itahitaji miaka mingi kwa nchi hiyo kurudi katika hali ya kawaida.



Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents