Habari

Mtikila alia na Richmond, Balali

Mwenyekiti wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila, amesema ana mpango wa kufungua kesi Mahakama Kuu wakati wowote kuanzia sasa dhidi ya tuhuma za ufisadi anaodai kufanywa na maofisa wa serikali waandamizi kupitia kampuni ya Richmond, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Kampuni ya simu (TTCL).

Na Lucy Lyatuu



Mwenyekiti wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila, amesema ana mpango wa kufungua kesi Mahakama Kuu wakati wowote kuanzia sasa dhidi ya tuhuma za ufisadi anaodai kufanywa na maofisa wa serikali waandamizi kupitia kampuni ya Richmond, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Kampuni ya simu (TTCL).


Mchungaji Mtikila aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.


Alisema utaratibu wa mambo hayo unaendelea vyema na kwamba wakati wowote kuanzia sasa kesi zitakuwa mahakamani na kwamba lengo lingine la chama chake ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anakuwa na uchungu na nchi yake.


“Ni lazima watu wawe na uchungu na mali zao ambazo zinapotea hovyo… Ndio maana DP hatukuwa na haja ya kuzungumzia sakata la BoT lililokuwa likiendelea Bungeni kwa kuwa tunajiandaa ili mahakama iweze kutoa haki,“ alisema.


Alisema ana wanasheria 11 wanaoendelea kukusanya nyaraka mbalimbali ili kuanza kulikabili suala hilo litakapofika mahakamani.


“Unajua wanasheria hao wanataka wawe wawili wawili, ndio maana wanaendelea na kukusanya nyaraka ambapo wengine wanashirikiana na wanataaluma waliopo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),“alidai.


Mchungaji Mtikila alisema hiyo itakuwa ni hatua moja ya kuwarudishia watanzania nchi yao na urithi wao ambapo mapambano yataanza kwa ari mpya nguvu mpya na kasi mpya.


Alisema kwa kutumia makahama atahakikisha kuwa Tume huru inaundwa na Bunge kwa ajili ya kuchunguza tuhuma za ubadhirifu katika BoT na pia kumchunguza Gavana wa benki hiyo, Bw. Daud Balali.


Hata hivyo, alisema anatabiri kutokea kwa mambo mabaya pindi mahakama itakapokwenda kinyume na uzalendo wa Watanzania walio wengi “kwani ni haki ya msingi ya kila mwananchi kufahamu utendaji wa kila sekta“.


Kupitia taarifa za inteneti, imekuwa ikidaiwa kwamba BoT ilitumia fedha nyingi kuliko inavyostahili katika ujenzi wa majengo mawili pacha ambapo inadaiwa kuwa sh. bilioni 40 kilifujwa kupitia akunti ya madeni ya nje.


Inadaiwa kuwa fedha hizo zililiwa na maofisa wa BoT kwa kushirikiana na wanasiasa waandamizi pamoja na wafanyabiashara wakubwa.


Akiongea na waandishi wa habari juzi, Bw. Balali alisema tuhuma zinazoelekezwa kwake ni chuki binafsi na hivyo hatarajii kujiuzulu. Alisema chuki hizo anahisi zinatokana na yeye kuwakatalia dhamana ya kukopa katika mabenki baadhi ya wafanyabiashara wakubwa na kwamba wamemua kumzushia tuhuma hizo kwa ajili ya maslahi yao binafsi.


Alisisistiza kwamba ataendelea kuchapa kazi kama kawaida na moyo wake ni mweupe.


Mwishoni mwa wiki iliyopita, wanaharakati wa asasi zisizo za kiserikali nchini, walimtaka Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Daudi Balali, kujiuzulu wadhifa huo ili kutoa fursa kwa uchunguzi huru kufanyika.


Nao walishauri kuundwa kwa Kamati ya Bunge ili kuchunguza tuhuma za ufisadi zinazoelekezwa kwake kama ambavyo imekuwa ikipendekezwa na baadhi ya wabunge.


Mchungaji Mtikila alisema wakati umefika wa kuitaka mahakama kutoa tamko juu ya notisi ya siku 90 iliyoandikwa Machi mwaka huu kwa ajili ya kuitaka serikali kurejesha Sh. bilioni 256 za TTCL.


Mtikila alisema kesi nyingine anayotazamia kufungua ni ya kutaka kufutwa kwa vifungu vya kisheria ambavyo vinawalinda marais wastaafu kutoshitakiwa.


Katika hatua nyingine, Mchungaji Mtikila aliwashauri viongozi wengine wa vyama vya siasa kuungana nae kwa ajili kwenda mahakamani kudai kile alichoita tume huru ya uchaguzi “kuliko kususia kushiriki Uchaguzi Mkuu ujao“.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents