Habari

Mtoto amfunga mama yake jela

MKAZI wa Kashai mjini hapa, Bw. Sylvanus Kagimbo (25), amesababisha mama yake mzazi Bi. Anath Abdumaliki (46), kuhukumiwa kifungo cha miezi sita jela na Mahakama ya Wilaya ya Bukoba, baada ya kukataa kuondoka katika nyumba inayodaiwa aliachiwa urithi na baba yake.



Na Mwandishi Wa Majira, Bukoba


MKAZI wa Kashai mjini hapa, Bw. Sylvanus Kagimbo (25), amesababisha mama yake mzazi Bi. Anath Abdumaliki (46), kuhukumiwa kifungo cha miezi sita jela na Mahakama ya Wilaya ya Bukoba, baada ya kukataa kuondoka katika nyumba inayodaiwa aliachiwa urithi na baba yake.


Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Bukoba, Bw. Ignatius Bashemela, baada ya kuridhika na upande wa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.


Akisoma maelezo ya kosa katika mahakama hiyo, Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Bw. Jumanne Ibrahimu, alidai kuwa tukio hilo lilitokea Juni 8, mwaka jana, katika kata ya Kashai, Manispaa ya Bukoba.


Bw. Ibrahimu alidai kuwa mama huyo, alikaidi kutii amri hali ya Baraza la Ardhi la Wilaya ya Bukoba, iliyomtaka kuondoka kwenye nyumba ambayo ni ya urithi, baada ya mtoto wake wa kuzaa kumkana, kuwa si mama yake mzazi.


Mama huyo alihukumiwa kifungo hicho cha miezi sita jela na kutakiwa kuondoka katika nyumba hiyo, baada ya kumaliza kifungo chake, baada ya mtoto wake kushinda mahakamani.


Ilidaiwa kuwa Sylvanus ni mtoto wa Bi. Anath wa kumzaa, lakini mtoto huyo alilelewa na mama wa kambo. Ilidaiwa kuwa kijana huyo, alikuwa akimtambua mama yake wa kambo kama mama yake mzazi, kutokana na mama wa kumzaa kumtekeleza.


Hata hivyo, mahakamani hapo ilidaiwa kuwa mtoto huyo alizaliwa na Bi. Anath, lakini kijana huyo ambaye anadaiwa kuwa kwa sasa anachukua mafunzo ya uaskari katika mkoa mmojawapo nchini, hamtambui mama huyo kama mzazi wake na hivyo haoni umuhimu wa kuishi naye katika nyumba aliyoachiwa urithi na baba yake mzazi.


Ilidaiwa kuwa kijana huyo alilelewa na mama wa kambo hadi kufikia umri alionao sasa. Hata hivyo, wakati mama huyo akienda gerezani kuanza kutumikia kifungo chake cha miezi sita, tayari ana watoto wengine.


Ana mtoto wa kiume aliyehitimu elimu ya msingi mwaka jana anayehitaji kusomeshwa na kuhudumiwa na mama huyo.


Aidha, hali ya mtoto kumshitaki mama yake na kumfunga, imepokewa kwa hisia tofauti na wakazi wa hapa, baadhi yao wanaoijua familia hiyo fika, wakidai kuwa kijana huyo alilelewa na mama yake mzazi, hadi kumsomesha sekondari.


Hata hivyo, wakati wa kutolewa hukumu dhidi ya mama huyo, mwanawe hakuwa mahakamani hapo, kwa kile kilichodaiwa kuwa yuko chuoni Moshi.


Aidha, kwa upande wa mama huyo, akizungumza na gazeti hili, baada ya kuhukumiwa kifungo hicho, alidai kuwa atakata rufaa kupinga hukumu hiyo na kuondolewa kwenye nyumba hiyo, kwa kile alichodai kuwa mwanawe wa kumzaa hawezi kumsababisha kuondoka katika nyumba ya mumewe, na ilhali ana watoto wengine ambao anawalea kwa wakati huu.


Mama huyo kwa sasa yuko katika pilika pilika ya kumwandaa mwanawe aliyechaguliwa katika chaguo la pili kujiunga na elimu ya sekondari katika shule ya Bilele mjini hapa.


Alisema kuwa alifungwa kifungo cha ndani, lakini hajui ni msamaria gani aliyemtetea hadi kupewa kifungo cha nje, ambacho kimemsaidia hadi kupata nafasi ya kumtafutia mwanawe huyo mahitaji ya shule, ikiwa ni pamoja na ada, ambapo kama angefungwa kifungo cha ndani, mwanawe huyo, asingeweza kwenda shule.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents