Michezo

Mtoto wa Kikwete na Nkamia watwaa medali za dhahabu Marekani

Mtoto wa Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya kikwete, Rashid Kikwete pamoja na mtoto Abdulrazak Nkamia ambaye ni mtoto wa Mbunge wa jimbo la Chemba, Juma Nkamia wameliletea sifa Taifa la Tanzania baada ya kushinda medali za dhahabu katika mashindano ya Genius Olympiad yaliyofanyika nchini Marekani.

Genius Olympiad ni shindano la kimataifa la mazingira linalofanyika kila mwaka katika chuo kikuu cha Oswego kilichopo mjini New York. Rashid ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu Kikwete amesema kuwa wamejifunza mambo mengi walipokuwa katika mashindano hayo nakuwataka wanafunzi wenzake kuacha kukata tamaa katika masomo.

Naye, Abdulrazak ambaye ni mtoto wa mbunge huyo amesema ushindi wao haukuwa rahisi kwa sababu kulikuwa na wanafunzi zaidi ya alfukumi na mbili (1,200) kutoka nchi 73 duniani kote ambao walishiriki katika mashindano hayo. Katika mashindano hayo Rashid na Abdulrazak wameshinda medali hizo katika kipengele cha Sanaa ya jamii.

Awali mwalimu mkuu wa shule ya Feza, Ali Yavuz, amesema kati ya wanafunzi 22 wa kitanzania walioshiriki kwenye mashindano hayo, wanafunzi watatu wamerudi na medali tatu za dhahabu na hivyo kuitangaza nchi kimataifa. Mbunge wa Viti Maalumu Mama Salma Kikwete ambaye ni mke wa Rais mstaafu alikuwa ni miongoni mwa viongozi waliokwenda uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl. JK Nyerere kwa kuwapokea wanafunzi hao na kuwapongeza.

“Nina fahari kubwa kuona vijana wetu wamefanya juhudi katika mashindano haya, lakini pia naipongeza shule yao ya Feza kwa kuwatengeneza wanafunzi hawa hatimaye kuonekana vizuri katika uso wa dunia,” amesema Mama Salma ambaye pia ni mama mzazi wa Rashid.

BY HAMZA FUMO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents