Siasa

Muafaka waimega CCM

CCMMUAFAKA wa kisiasa visiwani Zanzibar umeingia katika hatua mpya, baada ya kuibuka mvutano miongoni mwa wajumbe wa Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa

Na Waandishi Wa Mwananchi, Butiama, Zanzibar

 

 

 

MUAFAKA wa kisiasa visiwani Zanzibar umeingia katika hatua mpya, baada ya kuibuka mvutano miongoni mwa wajumbe wa Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM), kilichomalizika jana kijijini Mwitongo, Butiama, mkoani Mara.

 

 

 

Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho, zimeeleza kwamba ajenda ya muafaka imekuwa mwiba mchungu kwa wajumbe wa NEC wa upande wa visiwani hasa Unguja, wakipinga kuanzishwa kwa Serikali ya Mseto.

 

 

 

Vilevile taarifa hizo zimeeleza kuwa, kundi hilo limesema suala hilo halitawezekana, labda mwaka 2010 baada ya Uchaguzi Mkuu kufanyika nchini.

 

 

 

Wakati hali ikiwa hivyo upande wa Zanzibar, wajumbe wenzao wa NEC kutoka Pemba , wameonekana kutokuwa na mashaka na hatua hiyo wakieleza kwamba, itakuwa ukombozi kutokana na kile walichokieleza kuwa ni eneo hilo la Tanzania kuachwa nyuma kimaendeleo.

 

 

 

Hadi tunakwenda mitamboni, taarifa zinaeleza kwamba ajenda hiyo imeachwa ikajadiliwe na Wazanzibari wenyewe, ili waweze kuja na suluhisho litakalokuwa la kudumu kuliko ambavyo lingeachwa kuamuliwa na kikao hicho cha NEC.

 

 

 

Kuhusu ufisadi, suala hilo ambalo limekuwa likitikisa nchi katika maeneo yote, taarifa zimeeleza kwamba, limeachwa liendelee kushughulikiwa kisheria.

 

 

 

Kwa upande wa kutenganisha biashara na siasa, suala hilo, limebakia kiporo hadi hapo litakapotungiwa sheria ili kuepuka mgongano katika utekelezaji mzima wa masuala hayo.

 

 

 

Akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete alifafanua zaidi sababu za kufanyika Butiama na alikiri kuwa, kingefanya maamuzi mazito ambayo hayatahusu mageuzi ya kisera wala kiitikadi.

 

 

 

� Nalisema hili kwa sababu wapo watu wanaotumaini au wenye hofu kuwa hapa Butiama, kutatokea tamko la kurudia tena kutaifisha mali na kuziweka njia kuu za uchumi mikononi mwa dola. Wapo pia wanaodhani tutatoa tamko la kulirudisha nyuma gurudumu la mageuzi ya kisiasa yaliyoleta demokrasia ya vyama vingi na uhuru mkubwa wa watu kutoa maoni yao,” alisema.

 

 

 

Kikwete alifafanua kuwa, kikao hicho kingetatafakari hali ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama katika chama na taifa na kuwa katika kuzungumzia mambo hayo, yapo masuala makubwa yatakayojitokeza na kufanyiwa maamuzi.

 

 

 

Naye Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, amesema chama chake kinataka majibu ya uhakika kuhusiana na muafaka huo kutoka Butiama, unakofanyika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

 

 

 

Maalim Seif aliyasema hayo jana wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Garagara, Mtoni Mkoa wa Mjini Magharibi visiwani Zanzibar baada ya kukamilisha ziara yake ya kutembelea mikoa mitano ya Unguja.

 

 

 

Alisema katika kikao cha CCM kilichokutana Butiama juzi kujadili ajenda mbali mbali ikiwamo ya hali ya kisiasa ya Zanzibar na mazungumzo ya Muafaka kitatoka huko na majibu mazuri kwa wananchi kwa kuzingatia maslahi ya taifa na sio mtu binafsi.

 

 

 

Alisema CCM wamekwenda Butiama kupata mavumbavumba ya Mwalimu Nyerere kwa kuwa mwaka 1995, ndiye aliyependekeza kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, lakini waliokuwepo waliyapuuza maoni yake hayo.

 

 

 

Mwalimu Nyerere alipendekeza kwamba, njia pekee ya kupatikana ufumbuzi Zanzibar ni kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa lakini Rais Salmin (Komandoo) alipuuza na huyu Rais Amani naye amepuuza, alisema.

 

 

 

Akisisitiza suala la muafaka, Maalim Seif aliwaambia wanaCUF kuwa, CUF imemaliza kazi juu ya mazungumzo yake na wenzao (CCM), kutokana na kuwasilisha mazungumzo katika Baraza Kuu la Uongozi wa chama chake na hivi sasa kinachosubiriwa ni kauli ya Chama Cha Mapinduzi.

 

 

 

Nawaombeni jamani wacheni kuangalia maslahi ya mtu, lazima tuangalie maslahi ya nchi,� alisema.

 

 

 

Aliongeza kuwa, iwapo CCM haitakubali mazungumzo hayo dunia nzima itafahamu nani mchawi, kwa kuwa tayari CUF imetangaza kukubaliana na mazungumzo yaliyowakutanisha viongozi wa pande mbili.

 

 

 

Ikiwa CCM watakataa basi dunia nzima itafahamu nani mbaya kati yetu, na nani haitakii mema nchi yetu, � alisema.

 

 

 

Hata hivyo, aliwataka wananchi kusikiliza majibu kutoka ndani ya kikao cha CCM huko Butiama na kuahidi kwamba, CUF itatoa majibu baada ya kusikia kauli ya wenzao hao.

 

 

 

Akizungumzia utekelezaji wa muafaka huo, alisema wanaodhani kwamba chama kimeingia katika mazungumzo hayo, kwa lengo la kutaka madaraka au kuingia serikalini kwa mlango wa nyuma, wanakosea.

 

 

 

Kama kuna wana CCM wenye mawazo ya kuwa sisi tumeingia katika mazungumzo kwa ajili ya kutaka madaraka, wanakosea No� au wenye mawazo ya kuwa sisi tunaingia serikalini, kwa mlango wa nyuma�wanakosea sio suala la madaraka No..alisema.

 

 

 

Alisema lengo la kutaka kuingizwa katika serikali, ni kutaka kuwa karibu na utendaji wa serikali kwa Zanzibar na mazungumzo ya muafaka yamefanyika mara mbili, lakini utekelezaji wake ndio ulikwama, hivyo kuingia kwao watahakikisha waliokubaliana yanatekelezwa.

 

 

 

Alitaja jambo jingine la kutaka kuingizwa katika serikali ya Umoja wa Kitaifa kuwa, ni kuondoa uhasama na chuki zilizojengeka miongoni mwa wananchi kwa muda mrefu, ambapo baadhi ya wazee wamekuwa wakiwasusia watoto wao wanaojiunga katika chama cha CUF.

 

 

 

Seif, alisema kuwapo na serikali ya pamoja, kutaondoa migogoro isiyokwisha na kuweka sawa baadhi ya mambo, ikiwamo uendeshaji wa serikali yenyewe kwani ana imani kuwa, panapokuwa na umoja kheri na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu zitakuja.

 

 

 

Mimi ni muumini sana, naamini kabisa na nina hakika tukikaa pamoja, nchi yetu itapata baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwani hivi sasa hatupati baraka kutokana na mivutano na chuki zilizopo, alisisitiza.

 

 

 

Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents