Muafaka wanukia Kenya

Hali ya matumaini ya kurejea kwa amani imejitokeza tena nchini Kenya baada ya Rais Mwai Kibaki na kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM), Raila Odinga, kila mmoja kuteua wajumbe watatu kwa ajili ya kuanza majadiliano ya kutafuta amani.

Na NAIROBI, Kenya

 
Hali ya matumaini ya kurejea kwa amani imejitokeza tena nchini Kenya baada ya Rais Mwai Kibaki na kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM), Raila Odinga, kila mmoja kuteua wajumbe watatu kwa ajili ya kuanza majadiliano ya kutafuta amani.

 

Halikadhalika, imefahamika kwamba kikao cha Umoja wa Afrika (AU) kinachoshirikisha mataifa 53 ambacho kinatarajiwa kufanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia leo kitatumia muda mwingi kujadili ghasia zinazofukuta nchini Kenya.

 

Viongozi hao wawili ambao wamekuwa katika uhasama mkubwa tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu mwaka jana sasa wamekubaliana na mapendekezo ya Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (U.N.), Kofi Annan kutaka mfarakano huo umalizwe kwa njia ya majadiliano huku idadi ya watu waliouawa sasa ikikadiriwa kufikia 900.

 

Habari zilisema jana kwamba Rais Kibaki atahudhuria mkutano wa AU uliopangwa kufanyika nchini Ethiopia leo na kukanusha taarifa kwamba huenda asingehudhuria kutokana na ghasia zilizopo nchini mwake.

 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Bw. Moses Wetangula alikanusha pia madai kwamba kuhudhuria kwa Rais Kibaki katika mkutano huo ni kutaka kuhalalisha ushindi wake.
Alisema kwamba hadi sasa hakuna pingamizi lolote linalomzuia Rais Kibaki kuhudhuria kikao hicho cha AU kama Rais halali wa Kenya.

 

Mapema juzi, Katibu Mkuu wa ODM, Anyang N`yongo alitoa wito kwa nchi wanachama wa AU kuacha kuitambua serikali inayoongozwa na Rais Kibaki akidai kuwa siyo halali.

 

Wajumbe watatu kutoka vyama vya ODM na Party for National Unity (PNU) kinachoongozwa na Rais Kibaki walitarajiwa kuanza mazungumzo jana mjini Nairobi.

 

Taarifa za BBC zimesema kwamba mazungumzo hayo yatalenga katika kufanyia kazi haraka mapendekezo mbalimbali yaliyowekwa na timu ya Annan inayowajumuisha Rais mstaafu wa Tanzania, Bw. Benjamin Mkapa na mke wa Mzee Nelson Mandela wa Afrika Kusini, Bi. Craca Machel.

 

Bw. Annan amevipa vyama hivyo kipindi cha wiki mbili kuanzia jana kutafuta suluhu ya tofauti zao za kisiasa.
Akizungumza katika uzinduzi wa mazungumzo hayo uliowahusisha Rais Kibaki na Odinga juzi, Annan aliwasisitizia umuhimu wao wa kutafuta suluhu mapema kwa kuzingatia jinsi sifa za nchi hiyo zinavyoharibika.

 

Wajumbe wanaounda ujumbe wa PNU ni Waziri wa Sheria, Martha Karua, Mutula Kilonzo na Waziri wa Afya wa zamani, Profesa Samsoni Ongeri.

 

Kutoka ODM, wajumbe wanaoshiriki upatanishi huo ni William Ruto, aliyekuwa Balozi wa Kenya nchini Uingereza, Sally Kosgei na Makamu wa Rais wa zamani, Musalia Mudavadi.

 

Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, George Saitoti jana alionya kwamba jeshi la polisi halitaendelea kuona ghasia zikiendelea na kusisitiza kwamba barabara na njia za reli ziendazo nchi jirani zitaachwa wazi.

 

“Tumedhamiria kuwa wakali zaidi safari hii ambapo hatutaruhusu wahuni na wahalifu kufanya watakavyo. Hakuna nchi duniani inayoweza kuruhusu hali kama hii,“ aliwaambia waandishi wa habari mjini Nairobi jana.

 

Baadhi ya wananchi wa Kenya jana waliweka mashada ya maua katika “Kona ya Uhuru“ iliyopo mjini Nairobi huku kukiwa na baadhi ya kadi zilizosomeka “Uhuru“, “Upendo“ na “Samahani“.

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents