Muccos Nacho Chafungwa

Wanafunzi 1,178 wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Stadi za Biashara (MUCCoBS) cha mjini hapa, wamesimamishwa masomo kwa muda usiojulikana baada ya kugomea masomo.

Wanafunzi 1,178 wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Stadi za Biashara (MUCCoBS) cha mjini hapa, wamesimamishwa masomo kwa muda usiojulikana baada ya kugomea masomo, kufanya uharibifu wa mali na kuwashambulia wahadhiri kwa mawe katika vurugu zinazoendelea chuoni hapo kwa siku mbili mfululizo.

Uongozi wa chuo hicho uliwataka wanafunzi hao kuondoka chuoni hapo jana ifikapo jana saa 10 jioni na kwamba chuo hicho kitakuwa kinalindwa na polisi muda wote.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Suleiman Chambo, alisema wanafunzi waliosimamishwa ni wa mwaka wa kwanza, wa pili na wa tatu ambao wanadaiwa kuwashambuliwa wahadhiri kwa mawe na mchanga hadi kumjeruhi mmoja na kuvunja milango na mali nyingine za chuo hicho.

Alisema mgomo huo ulianza kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza kupinga ucheleweshaji wa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na kuishinikiza serikali kubadili sera ya utoaji wa mikopo hiyo kwa madai kuwa ina lengo la kuwabagua wanafunzi kwa misingi ya vipato.

Alisema kutokana na hatua hiyo, uongozi wa chuo juzi uliwasimamisha wanafunzi hao kwa muda usiojulikana na kutakiwa kuondoka chuoni hapo ifikapo saa 10 jioni, lakini wanafunzi hao waliitisha kikao na kurejea chuoni hapo nyakati za usiku kuwahamasisha na kuwashinikiza wanafunzi wengine kuunga mkono mgomo huo.

Alisema nyakati za usiku alitumiwa ujumbe wa simu ya mkononi uliosisitiza mgomo unaendelea uliosomeka kuwa: “Kesho ndo kesho, mwanaume hatishiwi nyau, mgomo upo pale pale, tuwaunge mkono mwaka wa kwanza, asubuhi hakuna kwenda darasani, tuwe pamoja wana MUCCoBS.“

Alisema kutokana na ujumbe huo, jana asubuhi wanafunzi wa mwaka wa pili na watatu wanaochukua shahada kugoma kuingia madarasani kwa madai ya kuunga wenzao mkono na kwamba kwa wale waliokataa walitolewa madarasani kwa nguvu na wale waliokuwa vyumbani nao walitolewa na kutakiwa kuunga mkono mgomo huo.

Profesa Chambo aliongeza kuwa wanafunzi wengine wanaochukua stashahada na cheti waliokuwa bwenini walivamiwa na kuporwa simu na kisha kutolewa kwa nguvu na kwa wale waliokataa walimwagiwa maji vyumbani.

Alisema wahadhiri watatu walioingia madarasani kufundisha walipigiwa kelele na kuimbiwa nyimbo mbalimbali hadi wakashindwa kuendelea na ufundishaji, huku wanafunzi wakirusha mawe na mchanga na kumjeruhi mhadhiri mmoja kwa fimbo.

Alisema wanafunzi na idadi yao kwenye mabano wanaochukua masomo ngazi ya cheti (161), stashahada (251) na shahada ya uzamili (108) hawahusiki na mgomo huo na kwamba wataendelea na masomo kuanzia leo huku wakilindwa na polisi kuhakikisha kuna amani na utulivu.

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents