Habari

Music Reviews: Doro (Walter Chilambo) & My Baby (Quick Rocka ft Ngwair na Shaa

Wiki hii Walter Chilambo na Quick Rocka wameachia ngoma zao mpya. Huu ni uchambuzi wangu kwa ngoma hizo.

page

Doro – Walter Chilambo (produced by Marco Chali, MJ Records)

Sina uhakika kama beat yote ya wimbo huu imetengenezwa Marco Chali ama pia mdogo wake (aliyeproduce Kesho ya Diamond) amehusika pia kwakuwa mwanzoni nasikia jina lake likitajwa. Doro ni miongoni mwa nyimbo nyingi zilizoandikwa na producer Marco Chali.

Ni idea aliyoiandika na kuingiza sauti kwenye beat hii inayopiga mithili ya nyundo inapogogengelea msumari kwenye mbao. Lakini kwakuwa Marco si mchoyo aliamua kumpa kazi hii kijana wake Walter Chilambo ili kumbadilisha kidogo kutoka kwenye nyimbo za taratibu kama ulivyokuwa wimbo wake wa kwanza, Siachi. Humu Marco amembadilisha kinoma Chilambo ambaye anazidi kudhihirisha kuwa alistahili kuwa mshindi wa EBSS mwaka jana.

Doro ni wimbo wa mapenzi ambao usipotulia unaweza usiuelewe haraka kwakuwa ni rahisi mno kutekwa na utamu wa melody ya wimbo pamoja na beat kali yenye gitaa linalocharazwa kwa umaridadi na kuifanya akili yako ishindwe kuyatafsiri mashairi. Kwenye Doro, Walter anamuimbia mpenzi wake anayeonekana kurudishwa nyuma na maneno ya wambea wanaoushambulia uhusiano wao. “Tamaa usikate hata wakisema mimi nikuache, sipaswi kuwa nawe, hawajui unanipa nini nidate,” anaimba Walter. Maneno hayo yanakuwa mwiba wenye nchakali unaochoma roho yake na yanayoonekana kuanza kumwelemea mpenzi wake.

Lakini Walter anamhakikishia kuwa anampenda sana na kwake amenoga kiasi ambacho hawezi kamwe kumwacha. Hivyo anamuuliza mbona uko doro? He is like.. ‘Tulia mama, mimi ni wako milele’. Doro ni ngoma kali sana na sipati picha ikipigwa kwenye spika kubwa ndani ya ukumbi wenye taa za rangi rangi, hakuna mtu anayeweza kuukwepa ushawishi wa beat hii inayoukuna mwili wako ujongee kwenye dancing flow. Hii naipa marks 8/10.

My Baby – Quick Rocka ft Ngwair & Shaa (produced by Manecky, AM Records)

Mara ya kwanza nimeusikia wimbo huu (jana usiku), ziliniijia sauti zilizomo kwenye wimbo uliomtoa Sean Kingston, Beautiful Girl (sikiliza kuanzia dakika 3:15) pale ambapo Sean Kingston anasindikizwa na sauti za miitikio yenye ladha ya nyimbo za kizamani. Simaanishi kuwa Quick ametoa idea hiyo huko, lahashaa lakini kuna sauti tamu zinazotambaa kwenye wimbo huu ambazo zimenivutia mno.

Honestly, kwangu My Baby ni miongoni mwa nyimbo bora kabisa zilizotoka mwaka huu. Nimeyaamini maneno ya Quick aliyoniambia wiki kadhaa zilizopita kabla wimbo huu haujatoka kuwa humo amebadilika kabisa na hivyo kuliongezea maana jina lake jipya la utani, Switcher.

Humu Quick ambaye jina lake halisi ni Abbot Charles amebadilika kiasi cha kumfanya aonekane kama ni muimbaji wa siku zote. Master J hakukosea kukichukua kipaji hiki. Naamini hata T-Pain ambaye wanafanana sana na Quick kwa muonekano wa sura, ataukubali uwezo wa pacha wake.

Tangu jana nauskiliza wimbo huu bila kuchoka na kila ninapousikiliza akili yangu inajaribu kunitengeneza picha ya uzamani hivi. Kwa mfano kijana wa enzi hizo (1950s) mwenye afro (ofcourse akiwa amebandika pia na chanuo), amevaa shati jeupe na suruali nyeusi ya kizamani, waliziita ‘fundi pima juu lakini chini kadiria mwenyewe’ (sijui kama nimepatia) ambayo chini imemwagika kama kile kitambaa cheupe cha mashine ya kusagia unga wa ugali (kama wewe ni mtoto wa kishua ni ngumu kukijua, mpaka uwe umewahi kutumwa kwenda kusaga unga enzi hizo, SMH!!!).

Halafu kijana huyo akiwa anasikiliza wimbo huu kwenye zile santuri za kizamani na akisnap his fingers huku akicheza ‘twist’. Ninaposikiliza wimbo kama huu, najiridhisha mwenyewe kuwa muziki wa Tanzania umekua sana. Kuanzia utunzi hadi production. Manecky amefanya kazi ya maana sana kwenye wimbo huu.

Laiti kama marehemu Ngwair angekuwa hai, huenda wimbo huu ungemsaidia kumrudisha kiasi kwenye ramani kwakuwa hadi anafariki dunia alikuwa akiendelea kustruggle kurudi na hit redioni. Ngwair amechana poa sana kwenye My Baby.
Siwezi kuacha kumpa sifa zake pia Shaa ambaye kama kawaida yake ameongeza utamu kwenye chorus ya wimbo huu kwa kuweka harmonies zilizoipa uhai. Naipa marks 9/10.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents