Habari

Muungano wa Afrika ‘AU’ waitaka DR Congo kuchelewesha matokeo ya mwisho ya Urais

Muungano wa Afrika (AU) umeitaka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo iahirishe kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu.


Wagombea wa uchaguzi mkuu DRC 2018 Martin Fayulu wa upinzani (Kushoto), Felix Tshisekedi (Kulia) na waziri wa zamani wa mambo ya ndani Emmanuel Shadary (Kati) –

Kwa mujibu wa BBC, Muungano huo unaonuia kuhimiza umoja na demokrasia, unasema una “shaka kubwa” na matokeo ya awali yaliotangazwa wiki iliyopita.

Matokeo hayo yalimpa ushindi mgombea wa upinzani Felix Tshisekedi lakini mpinzani wa utawala uliopo, Martin Fayulu, anasisitiza kuwa yeye ndiye aliyeshinda.

Matokeo ya mwisho yanatarajiwa kutangazwa leo Ijumaa.

Kumezushwa maswali mengi kuhusu uhakika wa matokeo hayo huku kukiwepo shutuma kwamba Tshisekedi anapanga mpango wa kugawana madaraka na rais anayeondoka Joseph Kabila.

Baadhi ya viongozi katika Muungano wa Afrika na serikali walikutana katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa jana Alhamisi na kutoa tamko kuhusu uchaguzi huo wa Desemba 30 unaopingwa pakubwa.

“Kumekuwa na shaka kubwa kuhusu namna matokeo ya awali yalivyokusanywa, kama ilivyotangazwa na tume huru ya kitaifa ya uchaguzi kwa kura zilizopigwa,” taarifa ya muungano huo imesema.

“Kadhalika, AU imetaka kuahirishwa kutangazwa kwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi mkuu huo,” iliongeza taarifa.


Felix Tshisekedi anaongoza chama kikubwa cha upinzani DR Congo kilichoanzishwa na marehemu babake mnamo 1982

Fayulu anatuhumu kwamba mshindi wa muda bwana Tshisekedi alikubaliana na rais anayeondoka Joseph Kabila.

Kabila amehudumu kwa miaka 18 na matokeo, iwapo yatathibitishwa, yataidhinisha ukabidhi wa kwanza wa uongozi kwa mpangilio tangu taifa hilo lipate uhuru kutoka kwa Ubelgiji mnamo 1960.

Tume ya uchaguzi imesema Tshisekedi alishinda 38.5% ya kura, ikilinganishwa na 34.7% alizoshinda Fayulu. Mgombea wa muungano wa serikali Emmanuel Shadary alijizolea 23.8%.

Fayulu aliwasilisha kesi katika mahakama ya katiba kupinga matokeo hayo Jumamosi akitaka kura zihesabiwe upya kwa mkono.

Matokeo hayo yanatarajiwa kutangazwa kama ni mapema sana leo, na wataalamu wanasema kuna uwezekano wa matokeo matatu.

Huenda mahakama:

  • Ikathibitisha ushindi wa Tshisekedi
  • Ikaagiza kura kuhesabiwa upya
  • Ikafutilia mbali matokeo yote na kuitisha uchaguzi mpya

Lakini mahakama haijawahi kubatilisha matokeo katika siku za nyuma.

Kutangazwa kwa Tshisekedi mshindi kumepingwa pia na kanisa katoliki lenye ushawishi mkubwa na ambalo pia linasema liliwatuma waangalizi 40,000 wa uchaguzi kote nchini.

Wataalamu waliopo katika serikali nchini Marekani, Ufaransa na Ujerumani pia wametilia shaka matokeo hayo.

akati huo huo, Umoja wa mataifa unasema, vita vya kikabila magharibi mwa Jamhuri ya Kidmeokrasi ya Congo vimesababisha vifo vya takriban watu 890katika muda wa siku tatu mwezi uliopita,

“Duru za kuaminika” zinaeleza mapigano kati ya jamii za Banunu na Batende yalizuka katika vijiji vinne huko Yumbi, ofisi ya Umoja wa mataifa kuhusu haki za binaadamu inasema.

Idadi kubwa ya wakaazi wa eneo hilo inaarifiwa wameachwa bila ya makaazi.

Uchaguzi mkuu wa Desemba 30 uliahirishwa huko Yumbi kutokana na ghasia.

Raia walioachwa bila ya makaazi ni pamoja na watu 16,000 waliotafuta hifadhi kwa kuvuka mto Congo hadi katika nchi jirani ya Congo-Brazzaville, umeongeza.

Nyumba 465 na majengo yaliteketezwa au kuharibiwa, zikiwemo shule mbili za msingi, kituo cha afya, soko na ofisi ya tume huru ya uchaguzi katika eneo hilo, Umoja huo umesema.

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents