Habari

Mvua kubwa yaathiri usafiri Dar Es Salaam, Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (MET) yaendelea kutoa angalizo kwa wananchi

Mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika mji wa Dar es Salaam, Tanzania imeathiri huduma ya usafiri wa umma huku idara ya hali ya hewa ikitoa tahadhari.

Kampuni ya Mabasi ya mwendo kasi (Udart) imelazimika kusitisha huduma zake usafiri kwa mabasi yanayotumia barabara kuu ya Morogoro eneo la Jangwani na barabara ya Kawawa katika Bonde la Mkwajuni kuelekea Morocco.

Taarifa ya Mkuu wa Idara ya Mawasiliano Udart, Deus Bugaywa imeeleza kuwa safari zilizositishwa ni kati ya Kimara -Kivukoni, Kimara – Gerezani, Morocco – Kivukoni na Morocco – Gerezani kuanzia mapema alfajiri ya leo Jumatatu.

“Huduma zinazotolewa sasa ni kati ya Kimara – Mbezi, Kimara -Magomeni Mapipa, Gerezani – Muhimbili, Kivukoni – Muhimbili na Gerezani – Kivukoni” amesema Buyagwa.Kito cha mabasi ya mwendo kasi katika eneo la jangwani

Eneo la Jangwani linafahamika kwa kujaa maji mengi barabarani kipindi cha mvua.

Udart wameomba radhi wateja wao na kuongeza kuwa wanaendelea kufuatilia hali ya maji Jangwani na kwamba yakipungua huduma zitaendelea kutolewa.

Baadhi ya watu wamekua wakitoa ushauri kwa wenzao walioshindwa kufika sehemu zao za kazi kutokana na changamoto ya usafiri ya kati kati ya mji kutumia usafiri mbadala.

Wengine waliamua kutumia mtandao wa kijamii wa Twitter kufanya hivyo.

Ukiachana kutatizika kwa usafiri wa mwendokasi, wakaazi wengine wa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam wamekubwa na adha kubwa ya foleni kutokana na mvua hizo kuharibu ama kuziba baadhi ya barabara muhimu.

Mamlaka zaonya mvua kubwa

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (MET) tayari imeshatoa tahadhari juu ya uwepo wa mvua kubwa ambayo itaupiga ukanda wa pwani wa nchi hiyo kwa siku tatu mfululizo kutokea leo Jumatatu Mei 13 mpaka Jumatano Mei 15.

MET wametahadharisha kuwa mvua hizo zitakuwa na madhara makubwa ikiwemo: “Baadhi ya makazi kuzungukwa na maji, ucheleweshwaji wa usafiri, kusimama kwa muda kwa baadhi ya shughuli za kijami. Kuanguka kwa kwa majani na matawi ya miti. Kuathirika kwa usafiri wa baharini na uvuvi.”

Mamlaka hiyo pia imetahadharisha kuwa kwa siku za Alhamisi na Ijumaa wiki hii, ukanda huo wa pwani ya Tanzania utakabiliwa na upepo mkali.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents