Michezo

Mvua ya fedha inayonyesha kwenye ligi ya China itaotesha mazao yao?

Mwaka 2016 umeonekana kuwa wa neema kubwa kwa wachezaji wa soka baada ya kuibuka soko jipya la kuvuna fedha za haraka kwa wachezaji – nayo ni ligi ya China.

Ni ukweli kuwa wachezaji wengi wanaotamani utajiri wa haraka wamekuwa wakivutiwa zaidi na soko la China kwakuwa wamekuwa wakilipwa fedha nyingi akiwemo Jackson Martinez, Alex Teixeira, Fredy Guarin na wengine lakini kwa wale wanaotaka kutengeneza historia binafsi kwenye mchezo huo wameonekana kuikataa safari hiyo ya mamilioni ya fedha akiwemo Cristiano Ronaldo.

Kwa sasa ligi hiyo ndio inaongoza kutoa wachezaji wanaolipwa mishahara mikubwa huku Carlos Tevez aliyesajiliwa siku chache zilizopita na klabu ya Shanghai Shenhua akitokea Bocca Junior ya Argentina akikalia kiti hicho kwa kupokea mshahara wa paundi laki 615,000 kwa wiki akifuatiwa na Oscar dos Santos wa Shanghai SIPG aliyetokea Chelsea akipokea 400,000 kwa wiki.

Hii si mara ya kwanza kwa matajiri wa ligi hiyo kumwaga fedha nyingi kama hizo. Miaka mitatu iliyopita waliingia na sera hiyo ya kusajili mastaa wakubwa wa Ulaya kwa ajili ya kuivutia ligi yao na walifanikiwa kuwasajili wachezaji kama Didier Drogba, Nicolas Anelka na wengine lakini baada ya muda waliamua kuwaachia kutokana na madai ya kufilisika kwa baadhi ya timu zilizokuwa zikiwamiliki mastaa hao.

Lakini kwa sasa wameonekana kujipanga vizuri zaidi kwa kuwa ni mfumo rasmi ambao umepangwa na serikali ya China ukiongozwa na Rais wao Xi Jinping ambapo anataka ligi yao iwe miongoni mwa ligi kubwa duniani zinazofuatiliwa kwa ukaribu huku wakija na sera nyingine ya kujenga viwanja vingi zaidi vya michezo.

Wachezaji wengine wengi wanatajwa kuwindwa kwenye ligi hiyo akiwemo Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, John Terry, Gareth Bale, Harry Kane, Neymar, Zlatan Ibrahimovic na wengine wengi huku makocha kama Antonio Conte wa Chelsea akitajwa kutakiwa kwenye ligi hiyo.

Mbali na kusajili wachezaji na kuwalipa mishahara mikuwa kwa sasa matajiri wa ligi hiyo wameamua kuviongezea nguvu ya ziada vilabu vyao kwa kusajili makocha wazito ambao pia wamewahi kuzifundisha timu kubwa za Ulaya akiwemo Luiz Felipe Scolari, Andre Villas-Boas, Sven-Göran Eriksson, Manuel Pellegrini na wengine.

Je wachina hao watafikia ndoto zao huku wakingozwa na sera ya kusajili mastaa wakubwa duniani kwa kuwavuta kwenye ligi yao ili kuongeza kachumbari kwenye ligi yao? Tuliona miaka michache iliyopita Marekani ilikuwa na mpango kama hiyo ya kuifanya ligi yao kuwa kubwa na waliwavuta wachezaji kibao wakubwa akiwemo David Beckham, Thiery Henry, David Villa na wengine lakini mwisho hawakufika walipokuwa wanapataka.

Macho ya mashabiki wengi wa soka ni kuona yale yanayosemwa kama kweli yataweza kutimia huku tukitegemea kuona mengi makubwa na yakushtua kwenye ligi ya China kwa mwaka huu mpya.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents