Habari

Mwalimu chupuchupu kuuawa na wananchi, wenzake wamnusuru kwa kumfungia na kufuli ofisini

Mwalimu wa Shule ya Msingi Mitonji katika Kijiji cha Mitonji Kata ya Mbuyuni katika Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, John Mandanda amenusurika kuuawa na wananchi wenye hasira kali, baada ya kuwacharaza viboko wanafunzi hadi mmoja kupoteza fahamu.

Image result for waziri wa elimu

Mwanafunzi huyo wa darasa la sita (jina linahifadhiwa) anadaiwa kupoteza fahamu kwa zaidi ya saa moja.

Kutokana na tishio la kuchapwa na wananchi hao walimu walimwokoa mwenzao kwa kumfungia ndani ya ofisi, huku wananchi hao waliotaka kumpa kichapo wakiwa wamebeba marungu, mashoka na silaa zingine za jadi.

Akizungumza na Nipashe jana kwa njia ya simu, Ofisa Elimu Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Elizabeth Mlaponi, alisema mwalimu huyo alifanya tukio hilo juzi majira ya saa 5:00 asubuhi wakati wanafunzi walipokuwa wakiingia darasani baada ya mapumziko mafupi.

Alisema mwalimu huyo akiwa shuleni hapo siku ya tukio, alitoa adhabu kwa baadhi ya wanafunzi ambao inaelezwa kuwa wanafunzi hao walikuwa wamechelewa kuingia darasani baada ya kengere ya kuingia darasani kupigwa, huku wakiwa nje ya darasa.

Mlaponi alisema mwalimu huyo baada ya kuona wanafunzi hao wamechelewa kuingia darasani, aliamua kuwacharaza viboko wanafunzi hao kila mmoja viboko viwili.

Alisema baada ya kutoa adhabu ndipo mmoja wa wanafunzi hao baada ya kuchapwa kiboko kimoja alianguka chini ya sakafu na na kumsababishia majeraha kwenye baji la uso wake.

“Tulipopata taarifa juu ya tukio hili la mwalimu kumchapa mwanafunzi na kumsababishia majeraha, tulifika hadi shuleni hapo na tulikuta wananchi wamezingira eneo la ofisi ya mwalimu mkuu ambapo alikuwa amefungiwa ndani na walimu wenzake wakimataka mwalimu huyu atolewe nje ili wampige,”alisema Mlaponi.

Afisa elimu huyo alieleza kuwa suala la mwalimu huyo wanaendelea kulishughulikia ikiwa ni pamoja na kulepeka katika ngazi za juu ikiwamo ofisi ya mkuu wa wilaya kwa ajili ya utekelezaji zaidi.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Mitonji, Shabani Nguseka, alisema ofisi ya serikali ya kijiji na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mitonji walipata taarifa hizo kutoka kwa baadhi ya wanafunzi wenzake wa shule hiyo wakieleza kuwa mwenzao amepigwa hadi kuzimia.

Mguseka alisema baada ya wananchi kupata taarifa hizo waliandamana hadi shuleni hapo na wakishinikiza kutaka mwalimu huyo wampe kichapo kama alivyomchapa mwanafunzi hadi kumsababishia kupoteza fahamu.

Alisema uongozi wa serikali ya kijiji ulishirikiana na familia ya mwanafunzi huyo kwa kumchukua mwanafunzi kumpeleka kwenye Zahanati ya kijiji cha Nagaga kwa ajili ya kupata matibabu ya awali.

Baba mdogo wa mwanafunzi huyo, Emmanuel Asili, alisema baada ya kupata taarifa hizo kuwa mtoto wake amepoteza fahamu baada ya kuchapwa kiboko, alilenda shuleni na kumkuta mwanae amepoteza fahamu, lakini alipoona akitokwa damu puani na masikioni ndipo alipochukua hatua za kumpeleka katika Zahanati ya Nagaga na baadae hospitali ya mji Masasi Mkomaindo.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu mwalimu Mandanda ambaye ndiye aliyemchapa kiboko mwanafunzi huyo, alikiri alifanya kitendo hicho, lakini alisema alimcharaza kiboko kimoja.

“Ni kweli nilimchapa kiboko kimoja na baada ya kumchapa nilimsikia akitamka maneno ambayo yalikuwa kama ni matusi hivi ndipo nilipopandwa na hasira, hivyo nikaanza kumpiga kwa kutumia mateke hivyo akaanguka sakafuni na kupata majeraha hayo,”alisema Mandanda.

Mandanda alisema ameamua kubeba gharama zote za matibabu za mwanafunzi huyo hadi pale atakapopata nafuu, na kwamba kutokana na tishio la kudhuriwa, ameamua kujificha yeye na familia yake.

SOURCE NIPASHE

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents