Mwanafunzi afungwa maisha

Mwanafunzi anayesoma kidato cha sita Zanzibar, Mohammed Hamza Mohammed (22), amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 13

Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar

Mwanafunzi anayesoma kidato cha sita Zanzibar, Mohammed Hamza Mohammed (22), amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 13.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu wa Mahakama ya Mkoa ya Vuga mjini Unguja, Bw. George Joseph Kazi.

Mwanafuzi huyo, mkazi wa Bububu, alipatikana na hatia baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka akiwemo daktari.

Hakimu Kazi alisema kulingana na ushahidi huo uliotolewa na daktari na mtoto mwenyewe, mahakama imeridhika nao.

Katika ushahidi wake, mtoto huyo alisema mshtakiwa alimsubiri njiani akitoka madrasa na kumchukua kwa nguvu hadi nyumbani kwake na kumfanyia unyama huo.

Alisema siku moja aliamua kukimbilia kituo cha polisi Bububu kutoa taarifa, baada ya mshtakiwa kumkamata kwa nguvu, ambapo askari walienda kumkamata na kumfungulia mashtaka.

Shahidi mwingine, Bw. Khatib Hassan Khatib, ambaye ni daktari, alithibitisha kuwa sehemu za haja kubwa za mtoto huyo zilipata michubuko, hali inayoonyesha aliingizwa kitu kigumu, kama vile uume.

Hakimu huyo alisema adhabu aliyotoa itakuwa fundisho kwa wale wote wenye tabia kama hiyo, lakini mshtakiwa ana haki ya kukata rufaa iwapo hakuridhika na uamuzi huo.

Kesi hiyo kwa mara ya kwanza ilifikishwa mahakamani hapo Januari 7, mwaka 2005.


 


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents