Habari

Mwanamke adaiwa kujifungua mtoto na kumnyonga

MWANAMKE wa Kijiji cha Saza wilayani Chunya, anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kujifungua mtoto wa kike na kumnyonga shingo wakati akiwa njiani kwenda kununua samaki Ziwa Rukwa.

Merali Chawe, Mbeya


MWANAMKE wa Kijiji cha Saza wilayani Chunya, anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kujifungua mtoto wa kike na kumnyonga shingo wakati akiwa njiani kwenda kununua samaki Ziwa Rukwa. Pascalia Joel (34) ambaye ni mfanyabiashara wa samaki, anadaiwa kumuua mtoto huyo kwa kumnyonga shingo baada ya kujifungua jana saa 5 usiku.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Suleiman Kova alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mwanamke huyo amepelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mwambani, Chunya kwa ajili ya uchunguzi. Alisema kuwa baada ya Pascalia kujifungua mtoto huyo wakati akiwa njiani kwenda Ziwa Rukwa kununua samaki, alimchukua na kumpeleka katika kituo cha afya cha Saza wilayani humo.


Baada ya wauguzi wa kituo hicho cha afya kumpokea mtoto huyo na kumkagua walimkuta akiwa amekufa huku shingo yake ikiwa imenyongwa, alisema. Alisema uchunguzi kuhusiana na kifo hicho unaendelea na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.


Wakati huo huo, watu watano wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kuhusika na matukio ya uhalifu, wakiwamo watu watatu wanaodaiwa kuwa ni majambazi ambao wanatuhumiwa kuhusika katika tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha.


Kamanda Kova aliwataja watu wanaoshikiliwa kuwa ni Lusajo Paul (28) maarufu kama Mwarobaini na Benson Mwambene (52) ambao wanadaiwa kuachiwa kutoka jela hivi karibuni pamoja na Tuntufye Mwalwisi (32), wote wakazi wa Kijiji cha Itumba wilayani Rungwe.


Wengine wanaoshikiliwa ni John Mwaitebele(34), Asangalisye Mwakembo (28) wote wa Katumba wilayani Rungwe ambao wanatuhumiwa kwa makosa tofauti ya kuiba transfoma na nyaya za simu. Kamanda Kova alisema kuwa Paul, Mwambene na Mwalwisi wanadaiwa kushiriki katika matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha Aprili 25 na 26, ambako inadaiwa waliwatisha raia kwa kutumia bunduki, kupiga risasi hewani na kisha kupora fedha, vocha na simu za mkononi ambazo idadi yake haikutajwa.


Alisema kuwa John Mwaitebele ambaye anadaiwa kuwa ni mfanyabiashara wa Katumba wilayani Rungwe, alikamatwa baada ya kuiba transfoma mali ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh milioni 3.5.


Inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alikutwa akiwa na mali nyingine za wizi ambazo ni nyaya mita 50 zenye ukubwa wa milimita 16, zinazodaiwa kuibiwa katika maeneo mbalimbali wilayani humo. Mtuhumiwa mwingine, Asangalwisye Mwankembo alikamatwa akiwa na nyaya mali za TTCL zenye urefu wa mita 500.Wote wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.


Wakati huo huo, Mahakama ya wilaya ya Rungwe, imemuhukumu mkazi wa Katumba wilayani Rungwe kutumikia kifungo cha miezi sita jela, baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa akiwa na lita sita za gongo.


Ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka Msaidizi wa Polisi, Juma Madenge kuwa Tuli Mwaijege (29) alikamatwa Mei 16 mwaka huu katika eneo la Katumba akiwa anauza pombe hiyo. Madenge alidai kuwa Mwaijege alikamatwa nyumbani kwake akiwa anauza pombe hiyo haramu asubuhi. Madenge aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mtuhumiwa huyo kwa kuwa vitendo vya uuzaji wa pombe haramu vimekithiri katika jamii.


Akisoma hukumu, hakimu wa Mahakama hiyo, Elia Mwakibete alisema kuwa licha ya mtuhumiwa kukiri kufanya biashara hiyo, anastahili adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine. Hakimu Mwakibete alimhukumu Mwaijege kulipa faini ya Sh 50,000 au kwenda jela miezi sita. Mtuhumiwa alishindwa kulipa faini hiyo na hivyo kwenda jela miezi sita.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents