Habari

Mwanasheria Mkuu apinga mgombea binafsi

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali amekata rufani kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuruhusu mgombea binafsi katika uchaguzi wa rais na wabunge.

Mwandishi Wa Habari Leo

 

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali amekata rufani kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuruhusu mgombea binafsi katika uchaguzi wa rais na wabunge.

 

Rufani hiyo iliwasilishwa katika Mahakama ya Rufani Jumatatu wiki hii, ikiwa ni wiki moja tu tangu Mwenyekiti wa Democratic (DP), Christopher Mtikila afungue kesi Mahakama Kuu kupinga uchaguzi mdogo wa Jimbo la Tunduru akidai unazuia wagombea binafsi kama ilivyoamuriwa na Mahakama Kuu.

 

Kwa mujibu wa maelezo yaliyowasilishwa katika rufaa hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali anaiomba Mahakama ya Rufani itengue uamuzi wa kuruhusu wagombea binafsi uliotolewa na majaji watatu wa Mahakama Kuu Mei 5 mwaka jana.

 

Hukumu hiyo inayoruhusu raia yeyote kugombea nafasi ya urais na ubunge bila kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa ilitolewa na Jaji Kiongozi Amir Manento na Majaji Salum Massati na Thomas Mihayo.

 

Katika rufaa hiyo Mwanasheria Mkuu alifafanua kuwa Mahakama Kuu ilikosea kisheria kutoa uamuzi huo kwa kupinga ibara za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania namba 21(1), 39 (1) (c) na 67 (1) (b) zinazotoa haki kwa rais kujiunga kwenye vyama.

 

Kwa mujibu wa maelezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mahakama Kuu ilikosea kwa uamuzi wake wa kuvifuta vifungu hivyo katika Katiba kwa kuwa iliacha mwanya unaowanyima wananchi mfumo wa kisheria wa kushiriki katika utawala wa serikali.

 

Aliiambia Mahakama ya Rufani kuwa Mahakama Kuu ilikosea kisheria kwa kutamka kuwa kushiriki uongozi nchini kama viongozi ni haki ya msingi ya kila mtu na kwamba haikuzingatia misingi ya uwakilishi wa uwiano.

 

Katika hukumu hiyo Mahakama Kuu ilimpa ushindi Mtikila kwa kusema kuwa mabadiliko ya sheria namba 34 ya mwaka 1994 yalipingana na ibara namba 21(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotoa haki kwa wananchi kujiunga katika vyama.

 

Katika hukumu ya Mahakama Kuu majaji walimpa muda Mwanasheria Mkuu kati ya siku ya hukumu na uchaguzi mkuu uliopita awe ameweka mfumo wa kuwezesha kuwapo kwa wagombea binafsi kwenye uchaguzi mbalimbali sambamba na wanaogombea kupitia vyama.

 

Hukumu hiyo ilikuwa ni ya shauri lililowasilishwa na Mtikila Februari 17, 2005 lililoiomba Mahakama Kuu itamke kuwa marekebisho ya sheria yalikuwa ni kinyume cha Katiba na kwamba alikuwa na haki kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 21 (1) kugombea urais au ubunge bila kupitia kwenye chama cha siasa.

 

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents