Habari

Mwanza: Wanawake wanne wauawa na kunyofolewa sehemu za siri

Siku moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela kuwaagiza wakuu wa wilaya za Kwimba na Misungwi kupambana na vitendo vya ubakaji na mauaji wanawake wanne wamekutwa wameuawa kikatili kisha miili yao kunyofolewa nyeti.

Miili ya wanawake hao ilipatikana jana ndani ya Shamba la Mifugo la Mabuki huku ikiwa na dalili za kunyongwa.
Mbali ya kupatikana kwa maiti hizo pia kwenye eneo la tukio kulikutwa mafuvu mawili ya binadamu. Kupatikana kwa maiti hizo kunafanya idadi ya wanawake waliouawa wilayani Misungwi kufikia wanane.
Juni 11 mwaka huu, wanawake wengine wanne waliuawa kikatili na watu wasiojulikana ndani ya pori hilo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amesema kuwa miili ya wanawake hao imeshatambuliwa hivyo akawataka wananchi kutoingia porini kukata kuni wakati Jeshi hilo likiendelea na uchunguzi wa mauaji hayo.
Alitoa mwongozo kwamba, katika hatua ya dharura wawepo askari ndani ya shamba hilo kwa ajili ya kufanya doria za kila mara, ikiwa ni pamoja na kuwasaka watu ambao wamekuwa wakiendesha matukio ya ubakaji na mauaji ndani ya eneo hilo.
Alisema miili ya wanawake waliouawa imetambulika kuwa ni Angelina Lumala (45), mkazi wa Kitongoji cha Ibelambasa, katika Kijiji cha Isakamawe, Kundi Laurent (35) na Mariamu Manila (30), wote wakazi wa Kitongoji cha Misasi na Ligwa Ngole (43), mkazi wa Kitongoji cha Bujingwa, Kijiji cha Mabuki.
Hata hivyo, taarifa za awali za uchunguzi zinadai wanawake hao wameuawa ndani ya siku mbili katika maeneo tofauti wakati wakiwa ndani ya shamba hilo la mifugo walipoingia kwa ajili ya kukata kuni.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Marco Peter aliwataka wanaume kuwalinda wake zao nyakati zote hususan wanapokwenda kukata kuni hivyo akaonya kwamba kwa sasa mwanamke atakapouawa, mtu wa kwanza kuwajibika atakuwa mumewe.
Katika muktadha huo, Peter aliwataka viongozi kuanzia ngazi ya kitongoji kuimarisha ulinzi wa Sungusungu.“Viongozi wa vitongoji na vijiji nao wanapaswa kuimarisha vikundi vya ulinzi wa jadi maarufu kama Sungusungu katika maeneo yao kwa ajili ya ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao,” amesema Peter.

Related Articles

One Comment

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents