Tragedy

Mzee Small afariki dunia, mwanae athibitisha kifo chake

Muigizaji maarufu Tanzania Said Ngamba maarufu kama, Mzee Small, amefariki dunia. Mzee Small alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Kiharusi kwa kipindi kirefu. Taarifa za kifo chake ni kwa mujibu wa mtangazaji na muimbaji Mike Lukindo aliyepewa taarifa na mwanae wa kiume.

mzee_small
Mzee Small alipokuwa mgonjwa

Kupitia Facebook, Mike ameandika:

Chanzo cha taarifa hizi ni Mtoto wake wa kiume Mahmudu (Mongamba) ambae amenipigia simu sasa hivi muda ni saa 7 usiku. Anasema Baba yake alipelekwa hospitali ya Muhimbili Jumamosi Tar 7 yani jana, muda wa saa mbili asubuhi baada ya kuzidiwa. Ameeleza kwamba alishinda nae kutwa nzima ila ilivofika saa 4:09 usiku akafariki akiwa mikononi mwake.

Mzee small alikua anasumbuliwa na tatizo la kupooza kwa muda mrefu. Mara ya mwisho mimi binafsi kumuona, nilienda kwake na Bambo, Zembwela pamoja na Team ya HOTMIX ya East Africa Television kumfania mahojiano. Alikua amechangamka lakini alikua anapoteza kumbukumbu kila anapoongea kwa muda mfupi. Sina ripoti zaidi ya hiyo kuhusu kilichosababisha kifo chake. Msiba wa Mzee small upo nyumbani kwake Tabata Mawenzi. Mungu ampumzishe kwa amani.

December mwaka jana Mzee Small alizushiwa kifo na kuzungumza na Bongo5 kuwa alipatwa na mshituko baada ya kupata taarifa kuwa kuna watu wanasambaza taarifa kuwa amefariki dunia, na kumlaani mtu aliyosambaza taarifa hizo za uongo.“Kwanza nawashukuru (Watanzania) na nawaheshimu kunipigia simu na kumtafuta mchawi, maana yake nyinyi ndiyo mumemvumbua mchawi,nawashukuru Radio zote,Tv zote nazishukuru mimi mzima bado nipo hai,” alisema.

“Kwanza mke wangu alishituka alafu mimi mwenyewe nilikuwa nimelala, lakini kwakweli mimi nilijisikia vibaya, namalaani huyo mtu,namlaani kwanzia leo mpaka kiama na mwenyezi mungu atamuona na kumsikia.” Naye mke wa Mzee Small alisema kwa upande wake ameathirika kwa kiasi fulani kwakuwa yeye ni muuguzi mkuu, alihitaji kuulizwa maendeleo ya Mzee Small kabla ya kutangaza taarifa za uongo. “Mimi ni mke wa Mzee Small kwakweli kwa tukio lililotokea limeniumiza sana kwasababu mimi ndiyo muuguzaji mkuu wa huyu bwana,niko nae inakuwa vigumu jambo kama hili linapotokea wakati mimi sijui chochote, kwakweli limeniumiza. Nawaomba Watanzania tufike mahala tuangalie, tusianze kusambaza vitu ambavyo hatuka ukweli navyo.”

Katika mahojiano aliyofanya November 13 mwaka 2012 kuhusu tatizo lililokuwa likimsumbua, Mzee Small alisema:

Mimi bado naumwa na ugonjwa wa “kiharusi” ambapo tangu tarehe 20 mwezi 5 mwaka huu mpaka leo hii kidogo nimekuwa napatiwa matibabu kwa matabibu wa tiba asilia. Ugonjwa huu niliupata wakati natokea Mwanza ambapo nilikuwa nimechukuliwa na mtangazaji mmoja, jina silikumbuki na kuwaburudisha kabla ya kusafiri kwenda nje ya nchi. Ugonjwa huu ulinipata asubuhi ya tarehe hiyo tano baada ya kurudi kutoka Mwanza ambapo baada ya kulala nilipoamka nikajikuta mwili unagoma kufanya matendo ya kawaida yaliyozoeleka kama kushindwa kuamka na kukaa kwenye kiti mwenyewe bila msaada wa mtu mwingine. Kuona hivyo mke wangu akanipeleka kwenye moja ya hospitali ya maeneo ya hapa Tabata Kimanga, ndipo walipogundua nina Kiharusi na daktari akanieleza nimepooza upande wote wa kushoto kwangu.”

Mzee Small anakuwa msanii mwingine wa filamu aliyefariki katika kipindi kifupi tangu waigizaji/waongozaji wa filamu Adam Kuambiana, Rachel Haule na George Tyson wafariki dunia.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents