Habari

Namba zote za simu kusajiliwa kukabili ujambazi

KATIKA mkakati wa kudhibiti matukio mbalimbali ya uhalifu nchini, namba zote za simu za mkononi zitasajiliwa katika benki maalum ya takwimu kuanzia mwaka huu wa fedha.

Na Theodatus Muchunguzi, Dodoma


KATIKA mkakati wa kudhibiti matukio mbalimbali ya uhalifu nchini, namba zote za simu za mkononi zitasajiliwa katika benki maalum ya takwimu kuanzia mwaka huu wa fedha.


Hatua hiyo ilitangazwa bungeni jana na Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Harith Mwapachu, wakati akiwasilisha makadirio na mapato ya wizara yake kwa mwaka wa Fedha wa 2007/08.


“Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kupitia utaratibu wa Public-Private Partnership imeundwa kamati ya wataalam ili kuimarisha usalama katika maeneo ya uwekezaji hapa nchini,” alisema Mwapachu na kuongeza: “Moja ya maeneo yenye kutishia usalama ni sekta ya mawasiliano ya simu za mkononi.”


Alisema simu hizo zimekuwa zikitumika kuwezesha kutenda makosa ya uhalifu kama utekaji nyara, ujambazi, vitisho, matusi na mengine.


Alisema makubaliano yamefikiwa kwamba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) mwaka huu wa fedha itaanzisha benki ya takwimu ili makampuni yote yanayouza simu za mkononi yaweze kuzisajili simu zote kwa kupata maelezo ya mtumiaji wa simu husika, na kujua nani mmiliki wa kadi au namba fulani ya simu.


Hata hivyo, waziri huyo alisema kufanikiwa kwa zoezi hilo kutategemea mambo kadhaa, ikiwemo namna makampuni yanavyofanya biashara ya simu yatakavyoshiriki katika zoezi hilo.


Kwa upande wake, Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama ilisema kuwa iliishauri serikali kwamba kuna umuhimu wa kuingilia mawasiliano ya simu ambayo polisi wanayatilia mashaka.


Akiwasilisha taarifa ya kamati, Mjumbe wake, Kanali Felen Mgeni, alisema hata hivyo, suala hilo lichukuliwe kwa umakini mkubwa ili kutoingilia uhuru wa watu na mambo yao ya ndani na pia kusababisha usumbufu kwa wageni (raia wa nje).


Mgeni alisema kuwepo na utaratibu wa sim-cards kununuliwa kwa usajili maalum badala ya sasa ambapo kila mtu ananunua popote na kutumia anavyotaka na kisha kuzitupa.


Mwapachu pia alisema wizara yake imejipanga kikamilifu kuondoa tatizo la ucheleweshaji wa upelelezi wa kesi kwa kuunda kamati maalum ya wataalam kutoka Makao Makuu ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ili kuchunguza malalamiko ya ucheleweshaji wa upelelezi wa kesi na kuchukua hatua za haraka kurekebisha dosari zitakazobainika.


Alisema kazi hiyo inaendelea kufanyika kwa wataalam hao kutembelea mikoa yote nchini na kufanya uchunguzi wa kesi za siku nyingi ambazo bado ziko mahakamani.


Kuhusu Sera ya Usalama wa Raia, Waziri Mwapachu alisema maandalizi yake yalianza Mei baada ya kupata mshauri ambaye ni Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na awamu ya kwanza itakamilika katika mwaka huu wa fedha.


Pia alisema hivi sasa wizara yake ipo katika mchakato wa kuandaa programu ya ya Maboresho ya Jeshi la Polisi chini ya usimamizi wa wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kushirikiana na maafisa wa Jeshi la Polisi na kuwa mchakato huo uko katika hatua nzuri ya utayarishaji.


Mwapachu aliyeomba jumla ya Sh147 bilioni, alisema chini ya programu ya maboresho ya sekta ya sheria, serikali iko katika mchakato wa kuhamisha shughuli za uendeshaji mashitaka kutoka Jeshi la Polisi na taasisi nyingine zilizokuwa zinafanya kazi hiyo na kuzipeleka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).


Katika maboresho hayo, Idara ya Upelelezi itagawanywa katika vitengo kulingana na utaalam wa makosa mbalimbali ya jinai. Kazi ya kuigawa idara hiyo itafanyika katika awamu mara baada ya maboresho ya Jeshi la Polisi kukamilika.


Katika hatua nyingine, baadhi ya wabunge wameelezea kukerwa na kuibuka upya na kwa kasi matukio ya ujambazi na kuitaka serikali iliwezeshe Jeshi la Polisi kwa vifaa na mbinu za kukabiliana na tishio hilo.


Wakichangia hotuba ya Waziri Mwapachu, wabunge hao walisema tukio la ujambazi lililotokea jijini Arusha wiki iliyopita ni fundisho kuwa vifaa vya kisasa na mafunzo ni muhimu kwa Jeshi la polisi.


Msemaji wa kambi ya upinzani, Ibrahim Muhammad Sanya (Mji Mkongwe-CUF), alisema: “Wakati umefika kwa jeshi letu la polisi kufanya kazi za ziada ili kuutokomeza ujambazi katika nchi yetu. Ule wakati wa kupongezana pongezana umekwisha, ni lazima usimamizi wa uchumi wetu uende sambamba na ulinzi wa uhakika kwa raia na mali zao. Hasa ukizingatia tunao wawekezaji wa ndani na wa nje.”


Sanya alisema katika matukio ya karibuni, imeonekana kuwa hali ya mipaka ya Tanzania sio shwari. Alisema hoja ni kwamba vipi raia kutoka nchi jirani kuingia na silaha nzito, na hata kupatikana na nguo maalum za kujikinga na risasi.


“Hivi wameingizaje bidhaa hizi hatari mipakani au tuseme wamezipata hapa nchini?” alihoji na kuongeza: “Leo vijana wetu wanafanya biashara ya kuingiza sukari kwa njia za panya huwa wanakamatwa mara zote kule mpakani Mbeya, lakini inashindikana kuwakamata raia kama hawa wa kigeni ambao hujiandaa kuja kufanya ujambazi.”


Alisema vile vile inawezekana fedha walizokamatwa nazo za Tanzania na za kigeni ndizo zinazotumika kuwahonga wananchi au hata baadhi ya askari wasio waaminifu ili wapate kutekeleza azma yao ya ujambazi.


Mbunge huyo alishauri kuwa ni vema Jeshi la Polisi likajipanga maeneo ya mipakani hasa upande wa Arusha kwani inaonekana kuna matetemeko sio ya tu ya ardhi, bali hata ya ujambazi.


Khalifa Suleiman Khalifa (Gando-CUF), alisema msingi wa mambo yote ya maendeleo katika nchi ni amani na utulivu. Alisema polisi wanakabiliwa na majukumu makubwa kama waliyonayo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika kulinda mipaka ya nchi.


“Ujambazi wa sasa kama uliotokea Njiro, Arusha ambapo silaha za kisasa na nzito zilitumika kama tunataka vijana wetu waende kupambana na majambazi na warejee na roho zao basi tuwawezeshe kwa mbinu na kwa vifaa.”


“Hali ya usalama inatisha. Tuongeze nguvu na nyenzo katika maeneo yote kwani ujambazi unatupunguzia imani,” alisema Mgana Msindai (Iramba Mashariki-CCM) na kuongeza kuwa Mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa ambayo matukio ya ujambazi yamerejea kwa kasi kubwa.


Kwa upande wake, Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama ilipendekeza kuwa ili kukabiliana na ujambazi Jeshi la Polisi liendeleze na kuimarisha mpango wa Polisi Jamii, serikali iimarishe operesheni za mara kwa mara katika maeneo yenye wimbi la ujambazi kama alivyofanya Kamanda Venance Tossi katika operesheni huko Kagera.


Pia imependekezwa helikopta za polisi zitumike kufanya doria za kushtukiza katika maeneo sugu kwa ujambazi pamoja na serikali kununua boti za ulinzi katika bandari na maziwa.


Grace Kiwelu (Viti Maalum-Chadema), alisema polisi wamejitahidi kudhibiti ujambazi lakini akasema tukio la Arusha la wiki iliyopita ni la kutisha na fundisho kuwa polisi wanahitaji vifaa vya kisasa kwani majambazi hao walikuwa na zana nzito, vikiwemo vifaa vya kujikinga na risasi.


“Vifaa hivyo ni muhimu kwani kazi inakuwa ni rahisi katika kupambana na ujambazi,” alisema Kiwelu.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents