Habari

NBS yashusha neema hii kwa watendaji wake

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imekabidhi kompyuta mpakato (laptop) kwa Ofisi zake za mikoa ili kuimarisha utendaji kwa kuongeza ufanisi na tija katika ukusanyaji wa takwimu rasmi na usambazaji wake kwa wakati.

Kompyuta hizo zilikabidhiwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi Dorothy Mwaluko wakati wa ufunguzi wa kikao cha Tatu cha Baraza la Tano la Wafanyakazi wa NBS kilichofanyika Dodoma.

Kutolewa kwa kompyuta hizo kunafuatia maombi ya Mameneja wa Ofisi hizo za mikoa ambayo waliyatoa wakati wa kikao cha watumishi wote wa NBS kilichofanyika hivi karibuni Mkoani Dodoma.

Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa NBS Dk. Albina Chuwa aliwataka watumishi wa NBS kuelekeza nguvu zao katika kutekeleza majukumu yao ya msingi na kwenda sambamba na kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya ‘Hapa Kazi Tu’.

“Kwetu sisi NBS kipaumbele chetu cha kwanza ni kazi, kipaumbele cha pili ni kazi na kipaumbele cha tatu ni kazi tu” alieleza Dk. Chuwa na kusisitiza watendaji wa Ofisi za mikoa kutokaa maofisini tu bali kujituma kutekeleza majukumu ipasavyo.

Aidha aliwataka watumishi hao kuhakikisha kuwa ukusanyaji wa takwimu unafanyika kwa wakati na kutolea mfano wa Takwimu za Mfumuko wa Bei za kila mwezi ambazo hutumika kupima kiwango cha mfumuko bei ambao hutolewa na NBS tarehe 8 ya kila mwezi.

“Mkichelewesha ukusanyaji wa takwimu hizi maana yake NBS tutashindwa kutoa mfumuko wa bei kitendo ambacho athari zake ni kubwa kwa nchi hivyo lazima tujitume kuhakikisha tunakamilisha kazi hiyo kwa wakati” Dk. Chuwa alisisitiza.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents