Habari

Nchi kuzalisha umeme megawati 2100

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli amekutana na timu ya wataalamu wa masuala ya umeme na ujenzi wa mabwawa ya maji ya kuzalisha umeme iliyotumwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn lengo ikiwa ni kubadilishana uzoefu na Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Rais Magufuli alikutana na pande zote hizo Ikulu, Dar es Salaam.

Katika mazungumzo na timu hiyo, Rais Magufuli alielezea nia yake ya kuhakikisha mawazo ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya tangu mwaka 1980 juu ya kuzalisha umeme kutoka maporomoko ya mto Rufiji, yanatekelezwa haraka iwezekanavyo.

“Sasa hivi nchi yetu inazalisha megawati 1,450 tu, lakini Stiegler’s Gorge itatuzalishia megawati 2,100. Umeme huo ni mwingi na utatusaidia katika viwanda, hivyo serikali tumeamua kutekeleza mradi huu,” ilieleza taarifa hiyo.

“Najua kutaanza kutokea vipingamizi mbalimbali, lakini naomba Watanzania tuwe na sauti moja, eneo litakalotumia ni kilometa za mraba 1,350 ambalo ni sawa na asilimia tatu tu ya eneo lote la Hifadhi ya Selous yenye ukubwa wa kilometa za mraba 45,000,” alieleza Dk Magufuli na kuongeza kuwa mradi huo utakuwa na faida nyingi zikiwemo uvuvi, maji kwa ajili ya wanyamapori na kilimo.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Naibu Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, Dk Medard Kalemani na timu ya wataalamu wa Tanzania wanaosimamia utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Power Project).

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents