Habari

Ndege yafuta safari yake baada ya mtoto mchanga kutovaa barakoa (+Video)

Safari ya ndege ya kampuni ya Canada WestJet ilifutwa na polisi kuitwa kwasababu mtoto alikuwa hajavaa barakoa. Safwan Choudhry anasema WestJet ilitaka mtoto wake mwenye umri wa miezi 19-avae barakoa, lakini mtoto huyo msichana aliendelea kulia.

Ndege hiyo inasema suala hilo si la mtoto, ambaye ana umri wa chini wa mtu anayetakiwa kuvaa barakoa, bali linamuhusu mtoto wa miaka mitatu Bwana Choudhry.

Jumanne asubuhi ndege chapa 652 iliyokuwa inatoka Calgary kuelekea Toronto ilisimamishwa na wasafiri wote wakaamrishwa kushuka.

“Ni kitu ambacho sijawahi kukishuhudia,” Bwana Choudhry aliiambia BBC.

Bwana Choudhry aliiambia BBC kuwa binti yake mkubwa, ambaye ana umri wa miaka mitatu, alikua anakula kitafunio kabla ya ndege kuondoka ndipo muhudumu wa ndege alipowakaribia akiwataka watoto wao wote wavae barakoa. Anasema yeye na mke wake walikuwa wamevaa barakoa.

Alisema aliomba kama mtoto wake anaweza kumalizia kitafunio, lakini wakasema walikuwa na “sera ambayo haiwezi kuvumilia hilo” na hawatafunga milango ya ndege bila yeye kuvaa barakoa. Bwana anasema alikubali kuvaa mara moja.

“Watoto wengi unahitaji kuwatuliza kwa namna fulani ambayo ndio njia ya kunyakua iPad kutoka kwao,”aliiambia BBC.

Alisema kuwa binti yake wa miaka mitatu alivaa barakoa, baada ya kumlazimisha kwa nguvu.

“Lakini binti yangu mdogo alikuwa na wakati mgumu, kimsingi alikuwa mgomvi.”

Bwana Choudhry anasema alikasirika sana hadi akatapika.

Anasema WestJet walikuwa wakali, na wakawaambia kwamba kwasababu binti yao mdogo hakuvaa barakoa, na amekasirishwa na kuvalishwa barakoa, familia yote itatakiwa kuondoka kwenye ndege.

Anasema, waliwaambia kwamba kama hawataondoka, wanaweza kukamatwa, kushitakiwa na kuadhibiwa kifungo cha gerezani.

Bwana Choudhry anasema yeye na mke wake walikuwa wenye heshima. Waliamua kukubali kuondoka kwenye ndege.

Baadaye aligundua kuwa kwa mujibu wa sera ya usafiri ya Canada, ni watoto wenye umri wa zaidi ya miaka miwili wanaotakiwa kuvaa barakoa, kwa hiyo binti yake mwenye miezi 19 hakupaswa kuvaa barakoa.

WestJet ilisema nini ?

WestJet ilikanusha kuwa binti yao mwenye umri wa miaka mitatu alivaa barakoa.

Ndege hiyo ilisema katika taarifa yake kwamba: “Kutokana na wazazi kushindwa kuonyesha ushirikiano wa kumvalisha mtoto wao mkubwa barakoa ambaye ana umri wa zaidi ya miaka miwili, wahudumu wetu waliwafahamisha watu wazima juu ya sheria ambazo tunatakiwa kuzifuata.

“Wahudumu wetu waliomba uwepo wa mamlaka baada ya wageni kukataa kutimiza agizo la mpito la usafiri na walikataa mara kwa mara kuondoka kwenye ndege .”

Video iliyochukuliwa kwa simu ya Bwana Choudhry inaonesha binti yake mkubwa akiwa amevaa barakoa , baada ya polisi kuwasili ndani ya ndege.

Anasema wakati baadhi ya wasafiri walikasirishwa na familia, watu wengi ndani ya ndege waliwaunga mkono. Wengi walizungumza wakiitetea familia hiyo changa, wakati bibi yao mdogo alipokuwa akilia, anasema.

Huo ndio wakati wahudumu wa ndege walipowaita polisi, alisema. Waliondoka ndani ya ndege, na hatimae safari ya ndege hiyo ilifutwa na wasafiri wakaondoka siku iliyofuata.

“Kutokana na kuongezeka kwa hali ya mtafaruku ndani ya ndege, wahudumu walihisi kutokuwa salama kuendelea na safari na safari ikafutwa mara moja ,” WestJet ilisema.

Katika video, afisa wa polisi aliwaelezea kuwa wakati suala la barakoa kuwahusu watu wazima ”lilitatuliwa”, “mienendo ya wasafiri wengine iliwafanya wahudumu wahisi kuwa hawako salama”.

Baadhi ya wasafiri wanasikika kwenye video ya tukio wakiwazomea polisi na wahudumu wa ndege.

Afisa baadaye alithibitisha kwamba wakati alipowasili, mtoto mkubwa alikuwa amevalia barakoa.

Polisi hawakuwasilisha mashitaka yoyote.

Msafiri mwenzake, Marian Nur, pia alirekodi baadhi ya majibizano na wahudumu wa ndege, kwasababu alihofia kuwa familia ilikuwa inalengwa kwasababu ya asili na dini yao – Mke wa Bwana Choudhry alikuwa amevaa hijab.

“Nilishituka sana, wazazi hawakupaza sauti zao juu, hawakukasirishwa na wahudumu , walikuwa wanajaribu kuwaelezea ni kwanini kumvalisha mtoto wao barakoa,” aliiambia CBC.

Bwana Choudhry anasema yeye na familia yake bado wapo Calgary, na hawajapewa ndege nyingine ya kwenda Toronto. Anasema anatumai yaliyompata hayatampata mtu mwingine tena.

“Watu wengi sana walipitia majonzi makubwa kwasababu ya ukosefu wa uelewa kwa upande wa sera” .

https://www.instagram.com/tv/CE8rjofjpHP/

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents