HabariUncategorized

Ndoto Hub yahitimisha mafunzo kwa wanawake wajasiriamali (Video)

Mradi maalum wa Ndoto Hub nchini wenye lengo la kuwawezesha vijana wakike kiuchumi kwa kuwapatia nyenzo za biashara za kibunifu, nafasi na maarifa ya kitaalamu yakufanyia kazi ndoto zao; imehitimisha mahafali yake ya pili kwa wanawake wajasiriamali waliojikita katika sekta ya kilimo-biashara, usindikaji wa vyakula na urejereshaji bidhaa.

Mahafali hayo yalifanyika kwa kushirikiana na balozi wa Siku ya Wanawake Wajasiriamali Duniani (Women Entrepreneurship Day) Tanzania, Bi. Imelda Lutebinga ambapo siku hiyo kwa Tanzania iliadhimishwa siku ya Ijumaa 7 Disemba 2018, ikiwa imebeba ujumbe Wanawake waongoza maendeleo kupitia teknolojia.

Mahafali hayo yalitanguliwa na maonyesho ya kazi na bidhaa mbali mbali zinazotengenezwa na wanawake wajasiriamali waliopata mafunzo kutoka Ndoto Hub, na baadae kufuatiwa na jukwaa la majadiliano lilioongozwa na Mgeni rasmi katika mahafali hayo Bi. Beng’i Issa, Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi.

Wazungumzaji wengine katika jukwaa hili ni pamoja na Bw. John Ulanga Mkurugenzi Mkuu wa TradeMark East Africa, Bi. Noela Bomani, Mwanzilishi-Mwenza wa iLearn East African pamoja na Bi. Diana Ninsiima Meneja Miradi na kiongozi wa masuala ya jinsia kutoka Digital Opportunity Trust Tanzania, jukwaa hili pia lilisimamiwa na Bi. Catherinerose Barretto ambaye ni mtaalam rasilimali watu na mwanaharakati masuala ya usawa wa kijinsia hasa katika uwanja wa teknolojia nchini.

Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Bi. Beng’i Issa alisema “tunawafariji na kuwahimiza wanawake wajasiriamali kupanua mitandao watu itakayowasaidia katika biashara zao na vilevile kuhusisha teknolojia ili kukuza masoko ya bidhaa na huduma zao. Aliendelea
kuwasihi wanawake hao kuhusu fursa mbalimbali za kujikwamua kichumi kwa kujitahidi kuendelea kujaribu na sio kuridhika mahala walipo. Alisema, kuna fursa nyingi za kuwawezesha wanacnhi kiuchumi ambazo zinaratibiwa na baraza la uwezeshaji wa
wananchi kiuchumi kupitia tovuti yao ya www.uwezeshaji.go.tz”

Meneja wa mradi wa Ndoto Hub, Bi. Tully Mwampanga amesema, ‘walihamasika kuanzisha programu hii kutokana na kuwepo kwa changamoto zinazowakabili wanawake wajasiriamali katika kuanzisha na kukuza biashara zao ndani na nje ya nchi.

Ndoto Hub inaamini katika kumuwezesha mwanamke ili kuleta maendeleo katika jamii yake na kuwa chachu ya maendeleo ya nchi kwa ujumla.’Bi. Tully pia alieleza kuwa mradi wa Ndoto Hub unajumuisha jitihada za wadau mbali mbali ambao wanajitolea
muda na uzoefu wao katika fani zao, kuwafundisha wanafunzi wanaopitia Ndoto Hub, hivyo kufanya mafunzo ya wiki 8 yanayotolewa Ndoto hub kuwa hai kabisa na sio nadharia tu.

‘Baadhi ya washauri na wakufunzi wetu hapa Ndoto hub ni watu waliofanikiwa sana katika fani zao katika sekta mbali mbali zikiwemo sekta za Masoko, Fedha na Utawala, Sheria na Uongozi’ aliongeza Bi. Tully.

Katika kuhitimisha mahafali hayo, Bi. Tecla Malulu, mmoja wa wahitimu wa Ndoto Hub alisema “leo ni siku ya furaha kubwa kwangu kwa sababu mimi na wanawake wenzangu tunaohitimu leo, tunasherehekea kuzishinda hofu zetu.” Bi. Malulu alielezea
jinsi mafunzo aliyoyapata Ndoto Hub yalivyomwezesha kupata mwongozo mzuri wa kujenga biashara yake. Bi. Malulu amesema Ndoto Hub imemjengea ujasiri, na zaidi imempa fursa ya kujitathmini na kujitambua na kuweza kufahamu mbinu bora zaidi za
kufanikisha biashara yake.

Alisisistiza kuwa anatamani wanawake wote wenye chachu ya maendeleo na kufanikiwa wangeweza kupitia katika program hii ya Ndoto Hub. Ndoto Hub inatoa nafasi nyingine ya mafunzo yatakayoanza Januari 2019 na inawakaribisha wanawake wote wenye mawazo ya ujasiriamali katika mchepuo wa Mitindo na Urembo (Lifestyle and Beauty) watume maombi ya kujiunga kupitia tovuti
www.ndotohub.com.

Ndoto Hub ni mradi ulioanzishwa na asasi ya Shule Direct inayomilikiwa nakuendeshwa na Bi. Faraja Kotta Nyalandu. Mradi huo umeanzishwa ikiwa ni hatua mojawapo ya kuunga mkono kwa vitendo sera ya Taifa ya Uwezeshaji Kiuchumi ya mwaka 2004 na katika kuleta maendeleo kufikia uchumi wa viwanda. Toka kuanza kwa mradi wa Ndoto hub mwezi Mei 2018 mpaka sasa mradi umeshafanikisha mafunzo kwa wanawake wajasiriamali 16 ambao wameweza kuanza biashara mbali mbali katika fani ya kilimo na usindikaji vyakula. Mradi wa Ndoto hub pia umepata ufadhili wa Fund for Internet Research & Education (FIRE) Africa na Raha Liquid Telecom.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents