Habari

NEC yakabidhi shilingi bilioni 12 kwa Rais Magufuli fedha zilizobaki kwenye uchaguzi mkuu mwaka jana

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekabidhi Sh bilioni 12 kwa Rais Dk. John Pombe Magufuli, zilizobaki baada ya uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais uliofanyika mwaka jana.

abilii

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva alikabidhi hundi hiyo kwa Rais Magufuli Dar es Salaam jana, taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, ilisema.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Jaji Lubuva alisema, “Mheshimiwa Rais fedha ambazo tunakukabidhi, tulijibanabana sana ingawa muda wenyewe ulikuwa mfupi lakini tulijibanabana sana bila kuathiri utendaji wa shughuli za uchaguzi.

“Isije ikawa inatoa sura kwamba iliathiri, haikuathiri, na katika hali hiyo kama ambavyo wengi ni mashahidi, hatujisifii, lakini uchaguzi ulienda vizuri,” aliongeza.

Akizungumza baada ya kupokea mfano wa hundi hiyo, Rais Magufuli aliipongeza NEC kwa kuokoa fedha hizo na kuzirejesha serikalini ili zipangiwe majukumu mengine.

Rais Magufulu azitaka taasisi nyingine za serikali ziige mfano huo wa uzalendo na kutanguliza maslahi ya taifa.

“Kitendo hiki ambacho mmekionyesha leo, kinaonyesha ni kwa namna gani Tume ya Taifa ya Uchaguzi chini ya uongozi wako Mheshimiwa Mwenyekiti ilivyo na watu makini na waadilifu sana. Kwa sababu hizi fedha ambazo kwa lugha uliyotumia ni bakaa, kutokana na zile ambazo mlipewa zaidi ya Sh bilioni 270, mkatumia Sh bilioni 261.6, mkabakiza Sh bilioni 12,” alisema Rais Magufuli.

“Mngeweza kuamua kusema hamkubakiza na hakuna mtu yeyote ambaye angewauliza, na saa nyingine pengine hakuna mtu yeyote ambaye angejua. Mngeweza pia kusema kiasi mlichotupa hakijatosha, tunaomba mtuongezee ama mngetengeneza maneno mazuri mazuri ya matumizi, bado nina uhakika serikalini wasingejua,” aliongeza.

Jaji Lubuva pia alimuomba Rais Magufuli aisaidie tume hiyo kupata jengo lake la ofisi kwa kuwa hivi sasa inatumia majengo ya kupanga ambayo yanaigharimu takribani Sh bilioni 1.4 kila mwaka kwa kulipia kodi ya pango, usafiri na gharama nyingine za uendeshaji.

Rais Magufuli amelikubali ombi hilo na kuamua kuwa fedha ambazo NEC imeziokoa zitumike kujenga ofisi ya tume, na amependekeza ofisi hiyo ijengwe mkoani Dodoma.

Rais Magufuli pia amelikubali pendekezo la tume hiyo la kuanzishwa mfuko wa tume ya uchaguzi ambao utakuwa unakusanya fedha kila mwaka kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaofuata.
Hatua hiyo itakuwa ni badala ya kuendelea na utaratibu wa sasa wa kusubiri mwaka wa uchaguzi ndipo zitengwe fedha zote za kugharamia uchaguzi huo.

Source: Mtanzania

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents