Habari

NEC yatoa fursa kwa waliopoteza vitambulisho vya kupiga kura

Tume ya Taifa ya uchaguzi(NEC), imesema kuwa wapiga kura waliopoteza vitambulisho vya kupigia kura watapata fursa ya kupiga kura kwenye uchaguzi mdogo wa Madiwani wa Kata 43 unaotarajiwa kufanyika Novemba 26, mwaka huu.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Bw. Ramadhani Kailima Mjini Dodoma ikiwa ni siku ya pili ya mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi yanayoratibiwa na kuendeshwa na NEC.

Bw. Kailima amesema wapiga kura hao wataruhusiwa kutumia vitambulisho vya uraia vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Hati ya kusafiria na leseni ya udereva.

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia kifungu namba 62 (a) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambacho kinasema mpiga kura aliyeandikishwa kwenye daftari atakwenda mwenyewe kwenye Kata aliyojiandikisha na kituo alichopangiwa” amesema.

Ameeleza kuwa hatua hiyo ni kumridhisha msimamizi wa kituo au msimamizi msaidizi wa uchaguzi kwamba yeye ndiye mpiga kura halali na kuongeza kuwa kifungu hicho kinamtaka mpiga kura aonyeshe kadi yake ya kupigia. Aidha, kinaeleza kwambaTume inaweza ikaelekeza utambulisho mwingine wowote utakao msaidia mpiga kura kuweza kupiga kura iwapo hana kadi.

Bw.Kailima amesema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia kifungu hicho, katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Novemba 26, 2017 imetoa maelekezo kwa wasimamizi wa uchaguzi kuruhusu wapiga Kura waliojiandikisha kwenye Dafatari la kudumu la Wapiga Kura kutumia Hati ya kusafiria, kitambulisho cha Taifa kilichotolewa na NIDA na leseni ya udereva.

Bw. Kailima amesema ruhusa hiyo imetolewa kwa sharti moja kwamba majina na herufi yaliyopo kwenye kitambulisho hicho yafanane na majina na herufi zilizopo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

Ameongeza kuwa NEC itakutana na vyama vya siasa hivi karibuni kuwajulisha juu ya maagizo hayo na kusisitiza kwamba tofauti yoyote itakayo kuwepo kwenye majina itamnyima mpiga kura fursa ya kupiga kura.

Bw. Kailima amesema maamuzi hayo yamefikiwa kutokana na kuwepo kwa changamoto kubwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ambalo kwa mara ya mwisho liliboreshwa mwaka 2015.

“Katika kipindi chote hichi (2015-2017) inawezekana kwa namna moja ama nyingine, kuna baadhi ya wapiga kura wamepoteza kadi zao za kupigia kura na kwa sababu hatuja boresha na sheria inasema watapata hizo kadi baada ya daftari kuboreshwa, wanaweza wakakosa fursa ya kupiga kura kwenye uchaguzi wa madiwani wa kata 43, lakini wengine kadi zao zimeharibika kiasi kwamba haziwezi kusomeka na wengine kadi zao zimechakaa kabisa kwa sababu moja ama nyingine kutokana na mazingira yaliyopo,” amesema.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents