Ngassa apewa miezi mitatu

Ngassa apewa miezi mitatu
Mrisho Ngassa amerejea nchini jana akitokea Uingereza alikokwenda
kufanya majaribio katika klabu ya West Ham United na amefikia katika
hatua nzuri

Inasemekeana kuwa Ngassa ameonyesha kiwango kizuri katika majaribio yake na benchi la ufundi limependekeza Ngassa kuungana na timu hiyo tena mwezi Julai mwaka huu watakapokuwa Italia kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa ligi na hapo ndipo itakapojulikana hatma yake.

Mmoja wa mawakala wa mchezaji huyo alisema kuwa benchi la ufundi la timu hiyo limeona kwamba mchezaji huyo akiendelea kubaki Uingereza na wao wakiwa wamebanwa na maandalizi ya mechi za lala salama za Ligi Kuu ya England itakuwa ni vigumu kwao kuendelea kumfanyia tathmini ya baadhi ya vitu inavyohitaji kumuangalia zaidi.

Hata hivyo, aliongeza kuwa katika kuonyesha kwamba mchezaji huyo amewavutia West Ham United, jopo la ufundi la timu hiyo litatuma wataalamu kuja nchini kumuangalia Ngassa katika mechi za kirafiki za timu ya taifa, Taifa Stars dhidi ya timu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nyingine ya New Zealand.

Aliongeza kuwa tofauti na awali, uongozi wa West Ham United pia umeahidi kwamba ndio utakaotuma tiketi ya mchezaji huyo kuelekea Italia kuungana na nyota wengine wa timu hiyo watakaokuwa huko.

Uongozi huo pia umempatia mchezaji huyo orodha ya vyakula anavyotakiwa kutumia na aina ya mazoezi ili kuweza kuujenga zaidi mwili wake.

Ngassa alisema kuwa anasikitishwa kusikia kwamba baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kwamba yeye ameshafeli majaribio hayo wakati shughhuli bado zinaendelea.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents