Habari

Ng’ombe watumika kuvutia wapiga kura, Serikali yaja na mpango wa kuwaanzishia wizara yake 

Waziri Mkuu wa jimbo la Madhya Pradesh Shivraj Singh Chouhan nchini India amesema kuwa serikali inampango wa kuanzisha wizara ya masuala ya ng’ombe hatua ambayo itachangia kuongezwa kwa fedha za kusaidia uhifadhi wake.

Mbunge na Waziri Mkuu, Shivraj Singh Chouhan 

Taarifa zinasema Bw Chouhan, ambaye ni wa chama cha BJP, amechukua hatua hiyo kama moja ya njia za kujaribu kumzidi mgombea wa chama cha upinzani cha Congress kila mmoja akijaribu kuwavutia wapiga kura wanaowathamini sana ng’ombe.

 

 

Chouhan alitoa tangazo hilo siku chache baada ya kiongozi wa chama cha Congress katika jimbo hilo Kamal Nath kuahidi kuanzisha makao ya kutoa hifadhi kwa ng’ombe iwapo chama chake kitashinda uchaguzi.

Amesema amesikitishwa sana na vifo vya ng’ombe ambao mara kwa mara hugongwa na magari wakivuka barabara katika jimbo hilo.

Chama cha BJP kimemshutumu mgombea huyo na kusema imekuwa ni sera ya chama cha Congress kutoa ardhi ya malisho kwa maskwota na hivyo kupunguza malisho ya ng’ombe.

Jimbo hilo limekuwa na bodi ya kuangazia maslahi ya ng’ombe inayofahamika kama Gau Samvardhan lakini Chouhan anaamini kwamba wizara ndiyo itakayofaa zaidi kutetea maslahi ya ng’ombe.

“Bodi hii inakumbwa na matatizo ya kifedha lakini kukiwa na wizara tatizo hilo halitakuwepo tena,” amenukuliwa na gazeti la Hindustan Times.

Ng’ombe hutambulika kuwa mnyama mtakatifu na waumini wa dini ya Kihindu walio wengi nchini India na kwamba mauaji ya ng’ombe ni haramu na kula nyama yake ni mwiko katika majimbo mengi ya India.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents