Michezo

Ngorongoro Heroes kuwafuata DR Congo leo usiku

Kikosi cha Wachezaji 21 na Viongozi 7 wa Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20 Ngorongoro Heroes wanatarajia kuondoka usiku kuelekea DR Congo kwenye mchezo wao wa marudiano wa kufuzu fainali za Africa kwa Vijana dhidi ya Timu ya taifa ya Vijana ya DR Congo safari iliyodhaminiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Ngorongoro Heroes inaondoka kwa kutumia Shirika la Ndege la Ethiopia ambapo kesho wanatarajia kufanya mazoezi kuelekea mchezo huo utakaochezwa Jumapili Aprili 22,2018.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) tunaishukuru Mamlaka Ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kujitokeza na kuidhamini timu yetu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20 Ngorongoro Heroes jambo lililotupa faraja kubwa.

TFF imekuwa na mzigo mkubwa wa kuzihudumia timu za Taifa ambao imekuwa ikiubeba na Taasisi kama Mamlaka ya Ngorongoro inapojitokeza kutusaidia kupunguza mzigo huo ni jambo la faraja na jambo la kushukuru.

Bado tunaziomba Taasisi mbalimbali na Makampuni kuweza kujitokeza kudhamini timu zetu za Taifa na mashindano mbalimbali yaliyo chini ya TFF.

Wadhamini wa Safari hiyo ya Ngorongoro Heroes Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kupitia kwa Kaimu Meneja wa Uhusiano Joyce Mgaya wamesema ni faraja kubwa kwao kuwa sehemu ya timu ya Ngorongoro ambayo wanaamini itafanya vizuri.

Bi Mgaya amesema huo ni mwanzo mwema kwao katika mahusiano hayo mapya na TFF kupitia timu hiyo ya Ngorongoro Heroes iliyobeba pia jina la Mamlaka yao ya Hifadhi.

“Tunaishukuru TFF katika mahusiano haya mapya ambayo yatatufanya na sisi kutoa mchango wetu katika timu hii ya Vijana ambao tunahakika wanakwenda kufanya vizuri katika mchezo huo na huu ni mwanzo tu kwa upande wetu” alisema Mgaya.

Naye Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes Ammy Ninje amesema maandalizi yanaridhisha na vijana wamepokea vyema mafundisho yake ikiwemo mfumo mpya wa namna ya kucheza na DR Congo ugenini.

Ninje amesema wanafahamu kazi iliyopo mbele yao lakini kwa maandalizi yaliyofanyika imani ni kubwa ya kufanya vizuri wakichagizwa na udhamini wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ambao wamejitokeza kuisafirisha timu hiyo jambo ambalo linawatia nguvu zaidi.

Nahodha wa kikosi hicho Issa Makamba amesema wachezaji wako tayari kwenda kuwakilisha vyema na wametiwa hamasa kubwa zaidi na morali kutoka kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Amesema wao vijana kazi yao ni moja kufanya vizuri kwenye mchezo huo kwa kupata matokeo yatakayowapeleka kwenye hatua ya raundi ya pili.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents