Habari

Ngorongoro, Tanapa,Tawa na Tawiri kuwa taasisi moja- Prof. Maghembe

Serikali inafikiria kuunganisha taasisi zote zinazohusika na sekta ya uhifadhi wa wanyamapori nchini kuwa chombo kimoja chenye nguvu kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji wa taasisi hizo pamoja na kuongeza ufanisi wa kiutendaji katika sekta hiyo muhimu hapa nchini.

Akizungumza bungeni mjini Dodoma, mwishoni mwa wiki wakati akihitimisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe alisema anaunga mkono ushauri uliotolewa na wabunge mbalimbali ukiwemo wa Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Atashasta Nditiye juu ya umuhimu wa kuunganisha taasisi hizo za uhifadhi.

“Wakati umefika sasa, tusiwe na makampuni (taasisi) zaidi ya manne ndani ya sekta hii ya wanyamapori, tuwe na kampuni (taasisi) moja tu ambayo itapunguza gharama katika uendeshaji, tutaunganisha jeshi la wahifadhi na jeshi hilo tutakalolitengeneza ni jeshi moja tu ambalo litakua na malezi chini ya jeshi la wananchi wa Tanzania, ili kujenga nidhamu, kuheshimu haki za binadamu na kufanya kazi kwa mujibu wa maslahi ya taifa,”. alisema Maghembe.

Aliongeza kusema “Jeshi hilo ambalo tunaliandaa kisasa,jeshi usu litakua na “chain ya comand” moja na litawajibika kijeshi kwa makosa ya haki za kibinadamu na usaliti wa taifa au usaliti wa uchumi wa
nchi yetu”.

Awali akiwasilisha bungeni hapo hotuba ya makadidirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake, Prof. Maghembe alizitaja taasisi hizo kuwa ni Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI).

Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) lilianzishwa mwaka 1959 kwa Sheria ya Hifadhi za Taifa Sura 282 na kupewa dhamana ya kusimamia na kuendeleza maeneo yaliyoanzishwa kisheria kuwa Hifadhi za Taifa.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents