Habari

NHC yakaidi amri ya Mahakama

LICHA ya Mahakama Kuu nchini kulitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kusimamisha kwa muda kutoza kodi mpya ilizopandisha, shirika hilo limeendelea kuwapelekea wateja wake ankara za kodi hizo mpya.

Maulid Ahmed


LICHA ya Mahakama Kuu nchini kulitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kusimamisha kwa muda kutoza kodi mpya ilizopandisha, shirika hilo limeendelea kuwapelekea wateja wake ankara za kodi hizo mpya. Wakizungumza na HabariLeo Jumapili, baadhi ya wapangaji wa shirika hilo wameonyesha ankara walizopelekewa na shirika hilo za kuwataka kuanza kulipa kodi mpya kuanzia Machi mwaka huu.


Kwa mujibu wa ankara hizo ambazo gazeti hili limezipata, mpangaji anatakiwa kulipa kodi mpya ya Machi na Aprili mwaka huu, pamoja na faini kwa wale ambao hawakuilipa kodi hiyo kuanzia Machi mwaka huu kama wanavyotakiwa Kuendelea kutoa ankara ya kodi mpya kwa wapangaji wa shirika hilo, kunapingana na amri ya Mahakama Kuu ya mwisho mwa mwezi uliopita ambayo imewataka shirika hilo kusimamisha kutoza kodi hiyo mpya wakati kesi ya msingi iliyofunguliwa na wapangaji hao kupitia Chama chao cha Wapangaji (TTA) inaendelea.


Mwezi uliopita, TTAilifungua kesikatika Mahakama ya Rufaa kupinga kodi mpya za nyumba zinazomilikiwa na NHC baada ya kutangaza kuwa utekelezaji wake ungeanza Machi Mosi mwaka huu.


Katika kesi hiyo namba 37/2007, Chama cha Wapangaji kiliitaka mahakama isimamishe kodi mpya iliyotangazwa na shirika hilo kutokana na kuonekana kuwakandamiza wapangaji na NHC ilazimishwe kuwa na majadiliano na wadau kupitia chama chao. NHC ilipandisha kodi za nyumba zake kuanzia Machi Mosi mwaka huu ikisema kuwa ni kutokana na kuzifanyia ukarabati na kuziboresha.


TTA katika madai yake ilisema NHC ilipandisha kodi za nyumba ndogo za eneo la Keko Dar es Salaam kutoka Sh 15,720 hadi Sh 35,000, za maghorofa ya Ilala kutoka Sh 19,500 hadi Sh 56,000, za maghorofa ya Amana kutoka Sh 20,000 hadi Sh 72,000 na mkoani Arusha kutoka Sh 27,000 hadi Sh 87,000 kwa mwezi. Akizungumzia madai hayo ya kukaidi amri ya mahakama, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Martin Madekwe alisema shirika lake linaheshimu amri ya Mahakama ya kusimamisha kodi mpya kwa muda.


“Kubadilisha ankara ni hatua ndefu hivyo wapo baadhi tumewapelekea ankara za kodi ya zamani lakini wapo waliopata ankara za kodi mpya …, kwa mtu mwenye busara ni bora alipe kodi mpya kwani hatujui atakayeshinda kesi. Kama wao watashinda basi fedha ya ziada aliyolipa itafidiwa,” alisema.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents