Michezo

Ni zamu yetu;Mwanariadha kinda aliyekimbia Mita 3000 ala shavu DSTV(+video)

MultiChoice Tanzania imetangaza kuendelea kudhamini mchezo wa riadha hapa nchini huku ikisaini makubaliano maalum ya kumdhamini mwanariadha kinda Francis Damiano Damasi. Udhamini huo unahusisha fedha ya kujikimu kwa mawanariadha huyo na mafunzo yake na wanariadha wengine katika kambi maalum ya mafunzo inayotarajiwa kuwa wilayani Mbulu.

Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa udhamini kwa mwanariadha huyo, Mkuu wa Mawasiliano wa MultiChoice Tanzania Johnson Mshana, amesema kuwa dhamira kubwa ya MultiChoice ni kuhakikisha kuwa mchezo wa riadha unakuwa na mchango mkubwa katika kuliletea taifa sifa, kutoa ajira kwa vijana wengi na kuchangia kikamilifu katika kukuza uchumi wa nchi.

“Tunataka taifa hili lijulikane ulimwengu mzima kama chimbuko la mabingwa, na tumeanza na riadha. Tumedhamiria kukuza mchezo huu na kuufanya kama chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana wetu, lakini pia riadha ni mchezo, ni burudani, na ni sekta nyeti kiuchumi kama ikiendelezwa” alisema Mshana na kuongeza “Tunataka kuusikia wimbo wetu wa taifa katika mashindano makubwa ya kimataifa, tunataka kuiona bendera yetu ikipepea juu katika kila mashindano makubwa ya riadha ya kimataifa, tunataka mamia ya vijana wetu wenye uwezo mkubwa katika riadha washiriki kwenye mashindano makubwa, waweze kujipatia kipato, kuwekeza na kuwa chanzo cha maelfu ya ajira na hatimaye kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi ya nchi yetu”

Amefafanua kuwa udhamini huo utakuwa wa mwaka mmoja na utaendelezwa na kuboreshwa kulingana na hali itakavyokuwa pamoja na mafanikio yatakayopatiokana. “ Huu ni mkakati wetu endelevu, ni mpango wetu maalum unaojulikana kama ‘Ni Zamu Yetu’! ambao umejikita katika kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana wetu katika riadha.” Amesema Mshana.

Mbali na kumdhamini Damiano, MultiChoice pia itadhamini kambi maalum ya mafunzo itakayokuwa wilayani Mbulu ambayo inatarajiwa kuanza mafunzo rasmi hivi karibuni. Amebainisha kuwa taratibu za kuanza kwa kambi hiyo zipo katika hatua nzuri na kambi inatarajiwa kuanza rasmi Agosti mwaka huu na itakuwa na wanariadha kinda wasiopungua sita – wasichana na wavulana.

Kwa upande wake mwanariadha Damiano ambaye ni mshindi wa medali ya shaba katika mashindano ya vijana ya Jumuia ya Madola yaliyofanyika visiwa vya Bahamas, amesema udhamini huo utamfanya aweze kufanya mazoezi yake vizuri kwani sasa hyo ndiyo itakuwa kazi yake ya kudumu. Amesema kilicho mbele yake ni ushindi tu. “Nashukuru sana kwa udhamini wa MultiChoice, na mimi naahidi kuwa nitafanya kila niwezalo kuhakikisha kuwa siwaangushi MultiChoice na siwaangushi Watanzania.”

Katibu mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania Wilhelm Gida-Buday, amesema wamefarijika sana kuona kuwa MUltiChoice inaendelea kudhamini riadha na akasema udhamini huo siyo tu utamsaidia mwanariadha husika, bali pia ni chachu hata kwa wanariadha chipukizi kuwa na moyo na ari ya kushiriki katika mchezo huo.

Amesema Shirikisho la Riadha Tanzania litahakikisha kuwa udhamini huo unakuwa wa manufaa na unazaa matunda yaliyotarajiwa ya kuleta medali zaidi kutaka katika mashindano ya kimataifa. “Ufadhili wa aina hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya mchezo wa riadha. Tunaahidi ushirikiano wetu wa hali na mali ili kufanikisha malengo na tutahakikisha kuwa tunatoa ushirikiano unaostahili kwa wadhamini wetu” alisema Gida.

Mwanariadha Francis Damiano Damasi, anatarajiwa kushiriki mashindano makubwa ikiwemo Mashindano ya vijana ya Afrika Mashariki yanayofanyika mwishoni mwa wiki hii jijini Dar es Salaam, Mashindano ya vijana ya Dunia (World Junior Championship) mwezi Julai nchini Finland, Mashindao ya vijana ya Olympic kanda ya Afrika mwezi Julai nchini Algeria, Mashindano ya vijan ya Olympic (Youth Olympic Games) mwezi Oktoba nchini Argentina, na mashindano ya nyika ya vijana (World Junior Cross-country) mapema mwakani nchini Denmark.


Mkuu wa mawasiliano wa MultiChoice Tanzania Johnson Mshana (wapili kushoto) na Kocha wa riadha Meta Petro (kulia) ambaye pia ni mlezi wa mwanariadha Francis Damiano wakisaini mkataba maalum wa udhamini wa mwanariadha huyo jijini Dar es Salaam. Multichoice imeingia mkataba wa mwaka mmoja wa kumdhamini mwanariadha huyo mchanga na pia kudhamini kambi ya mafunzo kwa wanariadha. Kushoto ni Katibu mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania Wilhelm Gida Buday na wa pili kushoto ni mwanariadha Fracis Damas Damiano


Mkuu wa mawasiliano wa MultiChoice Tanzania Johnson Mshana (kushoto) akimkabidhi nakala ya mkataba mwanariadha chipukizi Francis Damiano mara tu baada ya kusainia mkataba wa udhamini kwa mwanariadha huyo. Kulia ni Kocha wa riadha Meta Petro ambaye pia ni mlezi wa mwanariadha Francis Damiano. Multichoice imeingia mkataba wa mwaka mmoja wa kumdhamini mwanariadha huyo mchanga na pia kudhamini kambi ya mafunzo kwa wanariadha


Mkuu wa mawasiliano wa MultiChoice Tanzania Johnson Mshana (wapili kushoto) na Kocha wa riadha Meta Petro (kulia) ambaye pia ni mlezi wa mwanariadha Francis Damiano wakisaini mkataba maalum wa udhamini wa mwanariadha huyo jijini Dar es Salaam. Multichoice imeingia mkataba wa mwaka mmoja wa kumdhamini mwanariadha huyo mchanga na pia kudhamini kambi ya mafunzo kwa wanariadha. Kushoto ni Katibu mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania Wilhelm Gida Buday na wa pili kushoto ni mwanariadha Fracis Damas Damiano

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents