Habari

NIGERIA: Kodi ya harusi kufutwa baada ya wananchi kususia kuoa – Video

NIGERIA: Kodi ya harusi kufutwa baada ya wananchi kususia kuoa - Video

Mamlaka Kaskazini mwa Nigeria zimesitisha agizo lake la kuwakata watu kodi wanapooa baada ya wananchi wa eneo hilo kupigia kelele uamuzi huo. Uamuzi huo ulianza baada ya bwana Ado Sa’id, ambaye ni chifu wa kijiji cha Kera kaskazini magharibi mwa Nigeria, kutangaza kuwa kila mwanaume atakayetaka kuoa atapaswa kulipa kodi ya kiasi cha dola 375 za Kimarekani .

Hii ikiwa ni mbadala wa utamaduni ambao uliopo wa kulipa samani, vyombo vya jikoni na vitu vingine vya thamani kwa ajili ya kutoa kwa familia ya bibi harusi watakapofunga ndoa.

Kiongozi huyu amesema kuwa kulipa kodi ni rahisi zaidi kuliko kulipa mahari na itawafanya watu wengi kufunga ndoa kirahisi.

Amri hiyo iliwafanya wakazi wa eneo hilo kushindwa kufunga ndoa

Unaweza pia Kusoma kuhusu harusi:

Mwenyekiti wa kijiji cha Kano Maigida Adamu, amesema kuwa chifu alifanya makosa kwa kuanzisha kodi hiyo.

“Hakutuuliza kabla ya kutangaza kuanzisha kodi hiyo. Hivyo kuanzia sasa nimesitisa utaratibu huo na kuunda kamati ya watu saba kuangalia hatua ambayo chifu atachukua”, bwana Adamu aliiambia BBC.

Isah Yusuf,ambaye ni mkazi wa kijiji hicho amefurahia uamuzi uliotolewa na kusema kuwa jamii ilipinga kabisa jambo la kulipia kodi ndoa.

Hakuna mtu ambaye ameoa katika kijiji hicho na sasa miezi minne imepita tangu chifu Ado Sa’id, alipoweka malipo ya kufunga ndoa na kusitisha watu kupeleka vitu vya samani.

Chifu huyo alisema kuwa kulipa kodi ni rahisi zaidi na itawarahisishia watu wengi kufunga ndoa.

Harusi

Mwanakijiji mwingine ,Isah Kera, alisema kuwa sheria ile iliwalazimisha baadhi ya wapenzi kuhama na kwenda kufunga ndoa sehemu nyingine.

Sani Kera anasema kuwa ana watoto watano ambao wako tayari kuoa ,lakini mipango yao imebidi ihairishwe.

Harusi NigeriaTanzania:

Tanzania, ni nchi nyingine inayotajwa kushuhudia viwango vikubwa vya mahari katika baadhi ya jamii.

Huenda ndio moja ya sababu inayowafanya baadhi ya vijana kutooa kwa njia rasmi.

Vigezo ni vingi vinavyobaini kiwango cha mahari atkachotozwa kijana, mfano katika baadhi ya jamii – weupe wa msichana humaanisha mahari zaidi, lakini pia kiwango cha elimu cha msichana anyechumbiwa.

Kwa kukadiria kijana huitishwa ng’ombe au pesa zenye thamani ya kati ya shilingi milioni 5 hadi milioni 20 za Tanzania.

Uganda:

Utamaduni huu ni wa kawaida nchini Uganda, zaidi kwa jamii zilizopo katika maeneo ya mashinani, lakini pia hutolewa katika maeneo ya mijini.

Mahari nchini humu hufuata msingi ambao umekuwepo – kutoa kitu ili upewe mke.

Lakini sasa kuna mtindo kwa baadhi ya familia kuandikishana mikataba na bwana harusi kama ithibati ya kulipa mahari anayoitishwa.

Inaaminika kuwa iwapo mke amemtoroka mumewe baada ya kuteta na akarudi kwao, familia yake haina budi ila kurudisha mahari yote aliyolipiwa.

Mnamo 2010 mahakama nchini humo iliamua kuwa utoaji mahari ni halali, lakini majaji walipiga marufuku mtindo huo wa kurudishwa mahari wakati ndoa inapovunjika.

Kenya:

Katiba nchini Kenya haishurutishi ulipaji wa mahari, lakini ni jambo linalofahamika kuwa mahari hulipwa katika jamii tofuati nchini.

Baadhi ya jamii kwa mfano kwa wafugaji husisitiza mahari ya mifugo, huku kwa jamii nyingine mali, pesa taslimu na hata madini hupokewa kama mahari.

Huwepo hisia kwamba kuna malipo aliyotolewa mke kwenda kwa mume.

Mahari ni nini?

Utamaduni wa kutoa mahari upo katika nchi nyingi ulimwenguni zikiwemo barani Asia, mashariki ya kati sehemu kadhaa za Afrika na pia katika baadhi ya visiwa vya pasifiki.

Kiwango kinachotolewa hutofautiana kuanzia zawadi ndogo tu za kuendeleza utamaduni huo hadi maelfu ya dola za Marekani kwa mfano kama inavyoshuhudiwa katika ndoa za baadhi ya jamii.

Tangu jadi, utoaji mahari umekuwa ni utamaduni unaoheshimiwa na kuenziwa pakubwa hata miongoni mwa jamii za watu waliosoma na kuishi maisha ya kisasa.

Kwa kawaida mahari huwa ni kama mkataba wa makubaliano kabla ya ndoa ambapo mali kama ng’ombe, ngamia, mbuzi au hata pesa taslimu hulipwa na bwana harusi kwa familia ya bibi harusi ili apewe mke.

Iwapo mume hatotimiza mahari iliyokubaliwa kwa muda uliotolewa, kuna jamii ambao humrudisha mke nyumbani mpaka mume akamilishe kulipa mahari.

Chanzo BBC.

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents