Michezo

Nimeshinda, lakini nakiri ni kwa mbinde – Francis Cheka

Pamoja na kutwaa taji la mabara la WBF, Francis Cheka amekiri ushindi wake ameupata kwa mbinde kutokana na ubora wa mpinzani wake Geard Ajetovic katika pambano lao lililofanyika usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es salaam.
cheka.

Akizungumza na gazeti la Mwananchi, Cheka alisema mpinzani wake alimsumbua sana.

“Nimeshinda, lakini nakiri ni kwa mbinde mpinzani wangu alikuwa mbishi, amenipa wakati mgumu kwa kweli. Sikutarajia upinzani huu. Lakini nashukuru nimeshinda,” alisema Cheka.

Katika pambano hilo la raundi 12 lililosimamiwa na Rais wa WBF, Goldberg Haward, bondia Geard Ajetovic alicheza kwa kudhamiria kutwaa taji hilo hakumpa mwanya Cheka katika raundi ya tano hadi ya nane, hivyo kuwalazimu mashabiki wa Cheka kukaa kimya kwa dakika sita za raundi hiyo na wakuwapa nafasi mashabiki wachache wa Ajetovic.

Cheka alibadili raundi ya tisa na kumi huku raundi ya 11 na 12 mabondia hao wakicheza kwa kuviziana kabla ya Cheka kutangazwa bingwa kwa majaji 3-0. Jaji namba moja, Sakwe Mtulya alimpa Cheka pointi 115-112 wakati Anthony Rutha akitoa pointi 116-111 kwa Cheka na jaji namba tatu akitoa pointi 115-112 kwa Cheka kabla ya refarii kutoka Afrika Kusini, Eddie Marshall kumtangaza Cheka kuwa bingwa wa taji hilo katika uzito wa super middle.

Cheka ambaye yuko chini ya Kampuni ya Advanced Security Company Limited chini ya Mkurugenzi wake Juma Ndambile ambaye ni meneja wake, angeweza kupigwa kwa TKO kama si uvumilivu wa kucheza na kumaliza raundi zote 12 licha ya kupasuliwa na Ajetovic raundi ya nane na Ajetovic.

Akizungumzia ushindi wa Cheka, Ajetovic mwenye asili ya Serbia alisema mpinzani wake alipendelewa na kusisitiza yeye ndiye alistahili kushinda lakini uenyeji umembeba
Cheka.

“Nilistahili kushinda, lakini siwezi kupingana na uamuzi wa majaji, bado sijaamini kama nimepigwa na Cheka, Niko tayari kurudiana naye,” alisema bondia huyo aliyeambatana na kocha wake, Aksu Ahhysaidar

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents