Nizar aikacha Tottenham

Nizar aikacha Tottenham
Kiungo wa kimataifa wa timu ya Moro
United, Nizar Khalfan, atakwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya
kulipwa kwenye timu ya Vancouver ya Canada badala ya Tottenham
Hotspur`Spurs’ ya England

Awali, Nizar kati ya wachezaji wa
kutumainiwa katika kikosi cha timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars,
alikuwa akajaribiwe Tottenham, sasa ataelekea nchini Canada.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Moro United, Azim Dewji, Nizar
ametakiwa kwenda Canada kwa majaribio ya wiki mbili yatakayoanza Juni 8.

Dewji alisema, uamuzi huo umefikiwa na uongozi wa klabu hiyo na
mchezaji husika baada ya kufanya tathmini ya kina kulingana na hali
halisi ya ushindani.

“Kwa kuangalia hali halisi, Nizar anaweza kupata nafasi kwa
urahisi Vancouver kuliko Tottenham, hivyo tumekubaliana akaanzie Canada
ambako atapata mwanga zaidi wa soka,” alisema Dewji na kuongeza:

“Na kwa kuwa umri wake bado ni mdogo (miaka 21), bado
atakuwa na nafasi ya kujaribiwa katika klabu nyingine kubwa za Ulaya,
lakini baada ya kuwa ameshaivishwa Vancouver.

“Bado tuna mawasiliano na Spurs
na Moro United itaendelea kushirikiana nao.

“Kwa kuwa hii ni changamoto kwetu, tunarudia kusema sasa ni wakati wa
Moro United kuzama katika soka ya vijana. Mtazamo wetu utaanzia katika
kikosi cha msimu ujao wa Ligi Kuu,” alisisitiza Dewji aliyewahi kuwa
mfadhili wa Simba mwanzoni mwa miaka wa 1990.

Kwa upande wa Nizar, alikiri kuwapo kwa makubaliano hayo na
kusisitiza kuwa, anaamini njia itakuwa nyeupe kwake kama ataanzia
Vancouver kuliko Spurs.

“Hata mimi mwenyewe nadhani Vancouver nitafanikiwa. Waliniona hapa
nami nimeona uwezo wao, napata faraja kwamba inawezekana.

“Lakini ieleweke nako nitapita, kiu yangu ni kufika mbali kisoka, hasa kucheza katika moja ya ligi kubwa za Ulaya.”

Nizar anatarajiwa kuondoka wakati wowote wiki hii, baada ya kupata viza ya kuingia Canada tayari kwa majaribio kuanzia Juni 8.

Aidha, uongozi wa Moro United, unamtakia kila la kheri kwani mafanikio ya Nizar, ni mafanikio ya soka ya Tanzania.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents