Habari

NMB yatoa msaada wa mabati kutekeleza agizo la Waziri Mkuu

Benki ya NMB imetoa msaada wa mabati 400 kwa Wilaya ya Urambo Mkoani Tabora, lengo likiwa kuhakikisha inaunga mkono utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilolitoa kwa mikoa yote nchini yenye upungufu wa vyumba vya madarasa kuhakikisha ifikapo Februari 28, 2021 vinajengwa.

Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Angelina Nkwingwa akipokea msaada wa mabati yenye thamani ya Shilingi Milioni 15 kutoka kwa Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi Sospeter Magese kwa ajili ya kumaliza ukarabati wa shule tatu zilizopo wilayani humo. Hii ni sehemu ya jitahada za benki hiyo kuunga mkono utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilolitoa kwa mikoa yote nchini yenye upungufu wa vyumba vya madarasa kutatua tatizo hilo. Kulia ni Mbunge wa Urambo Margaret Sitta.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo Disemba 7, 2020 wakati akizungumza na Wakuu wa Mikoa, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI ili kuhakikisha wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaanza masomo.

Katika kikao hicho Waziri Mkuu Majaliwa Waziri Mkuu aliagiza Ofisi ya Rais-TAMISEMI ihakikishe kazi hiyo inakamilika kwa wakati na aliwataka watendaji hao wahakikishe ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa na utengenezaji wa madawati vinafanyika usiku na mchana.

Ili kuhakikisha agizo hilo la Waziri Mkuu linatakelezwa kwa haraka, Benki ya NMB imetoa msaada huo jana kwenye Wilaya ya Urambo, ambapo thamani ya mabati hayo ni sh. Milioni 15.

Akikabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Angerina Nkwingwa , Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi Sospeter Magese, alisema kuwa mbali na kurejesha sehemu ya faida kwa jamii benki hiyo imeona kuna haja ya kuunga mkono utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu.

Magese alisema mara baada ya kusikia wito wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  akisisitiza kwamba wanafunzi wote waliofaulu kuingia kidato cha kwanza lazima waanze masomo hawakusita kutoa msaada kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa.

“Kupitia msaada huu ambao benki ya NMB imetoa kwenu, ni matumaini yetu kuwa wilaya hii inaenda kutekeleza agizo la Waziri Mkuu, kwa wakati na kwa haraka kama ambavyo aliagiza na wanafunzi waweze kuanza masomo,” alisema Magese.

Akipokea msaada huo Mkuu wa Wilaya hiyo, Angerina Nkwingwa ameishukuru benki hiyo kwa kuendelea kuwasaidia wananchi na kueleza kuwa NMB imemwondolea aibu kwa kumvika nguo, na kuwa msaada huo umefika wakati mwafaka na kuwataka wadau wengine kuiga benki ya NMB.

Mkuu huyo wa Wilaya amewaonya wanafunzi kutotumia meza na viti  ili vidumu kwa muda mrefu kutokana na tabia ya baadhi yao kupanda juu yake na kusababisha kuharibika.

Wakati huo huo, Benki hiyo imetoa msaada wa dharura wa vifaa mbalimbali kwa wakazi wa kijiji cha Kipera na Kitongoji cha Kinyenze kata ya Mlali Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro baada ya kaya 54 kuathirika na mvua iliyoambatana na upepo mkali kuezua mapaa na kubomoa nyumba Januari 9, 2021.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa mkuu wa wilaya hiyo katika kijiji cha Kipera mkoani hapa, Meneja wa benki hiyo kanda ya mashariki, Dismas Prosper alisema kuwa baada ya kupata taarifa ya wakazi hao kupata janga hilo, benki hiyo imetoa msaada wa dharura wenye thamani ya sh. Milioni tano.

Dismas alisema kuwa vifaa hivyo ni pamoja na madogoro 54, mashuka 110, mchele kilo 540, lita 110 ya mafuta ya kula na sukari 160 kwa ajili ya kugawiwa kwa walengwa katika kipindi hiki kigumu.

“NMB imekuwa ikitoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa jamii hasa wanapopata janga mbalimbali na leo tumetoa vifaa muhimu vyenye thamani ya sh5milioni ambapo tunaamini uongozi utawagawia walengwa katika kipindi hiki kigumu,” alisema Dismas.

Afisa mtendaji wa kata ya Mlali wilaya ya Mvomero, Anuciata Mpina alisema kuwa Januari 9 mwaka huu mvua kubwa iliyoambatana na upepo ilinyesha na kusababisha madhara kwa kaya 54 ambapo nyumba zimebomoka na kuezuliwa mapaa huku watu 318 wakikosa makazi.

Mkuu wa wilaya ya Mvomero, Albanus Mgonya alisema kuwa baada ya kutokea kwa janga hilo kamati ya ulinzi na usalama ilitembelea nyumba za waathirika 318 na kuwataka watu wote ambayo wamekumbwa na janga hilo wasirejee katika nyumba ambazo zimebomoka upande mmoja.

Mgoya aliishukuru NMB kwa msaada huo ambao unaenda kuwaokoa wananchi ambao walikumbwa na janga hilo, ambalo alieleza limewaacha bila ya chakula ambacho walikuwa wameweka akiba.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents