Habari

“Ntampigia simu Waziri Ummy ‘Ambulance’ moja lazima alete hapa”-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (+video)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupeleka gari la kubebea wangonjwa katika kituo cha Afya cha Kibaoni kilichopo Halmashauri ya Mji wa Ifakara ili kuwapunguzia wananchi gharama ya kukodi gari kwa sh. 800,000 pale wagonjwa wao wanapopata rufaa.

“Nitampigia simu Waziri (wa afya) Ummy (Mwalimu) katika mgao ujao alete gari la wagonjwa hapa,” amesema Majaliwa

Pia, Waziri Mkuu ameielekeza Ofisi ya Rais-Tamisemi ihakikishe katika mgawo wa ujenzi wa hospitali za wilaya, Halmashauri ya Mji wa Ifakara ipewe kipaumbele kwa sababu eneo hilo ni kubwa na lina watu wengi lakini hakuna hospitali ya wilaya hivyo kusababisha msongamano mkubwa katika kituo cha Afya cha Kibaoni.

“Nimetembelea mwenyewe kituo cha Afya cha Kibaoni na nimeshuhudia msongamano wa wagonjwa, mgao wa pili wa ujenzi wa hospitali za wilaya Mji wa Ifakara lazima upewe kipaumbele. Suala la huduma za afya ni suala nyeti, hivyo ujenzi wa hospitali hiyo ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.”

Awali, Mganga Mfawidhi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Dk Happyness Ndosi alisema kituo cha Afya cha Kibaoni kinapokea na kuwahudumia wagonjwa wa  nje 225 hadi 250 kwa siku na wagonjwa wanaolazwa ni kati ya 50 hadi 80 kwa siku. Wakinamama wanaojifungulia kituoni hapo ni 400 kwa mwezi.

Akizungumzia kuhusu changamoto zinazokabili kituo hicho alisema kina upungufu wa watumishi 92, kwani kina jumla ya watumishi 83 huku mahitaji yakiwa ni watumishi 175,  ukosefu wa gari la wagonjwa na pia hakina gari lolote la kutolea huduma zikiwemo za chanjo, na usambazaji, uchakavu kwa baadhi ya majengo kama la wagonjwa wa n je.

Pia, kituo kinakabiliwa na ukosefu wa jengo la kutunzia watoto njiti, watoto wachanga na wale wanaohitaji uangalizi maalumu baada ya kuzaliwa (neonatal unit), ufinyu wa chumba cha kujifungulia pamoja na ukosefu wa mashine ya kutolea dawa za usingizi (anesthesia machine).

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali haitokuwa na msamaha  na watendaji wa halmashauri watakaobainika kutafuna fedha za makusanyo ya mapato ya ndani pamoja na fedha zinazotolewa kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye maeneo yao.

”Fedha za mapato ya ndani hazitumiki vizuri watu wanadukua mifumo, wanapaswa watambue kwamba Serikali ipo makini wakati wote. Watumishi wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo vya ubadhilifu hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.”

“Watumishi wa umma mnatakiwa kutekeleza majukumu yenu kwa weledi,” amesema Waziri Mkuu amesema watumishi wa umma wanatakiwa kujiepusha na  migogoro kwa kuwa ni kinyume na taratibu za kiutumishi.

“Haiwezekani viongozi wakagombania zabuni zitokanazo na fedha za kodi za wananchi, kwa ajili ya maslahi yao binafsi. Serikali itasimamia zabuni zote,” amesema

Chanzo Mwananchi

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents