Nyashinski alivyogeuka almasi kutoka mchangani

Mwaka wa 2015 msanii Nameless alipotangaza ujio wa Nyashinski kupitia kazi ya pamoja waliyoifanya ambayo ilifahamika kwa jina la ‘Letigo’ aliwatia mashabiki shauku kubwa ya kutaka kumsikia tena mkali huyo baada ya ukimya wake wa takriban miaka 9 kwenye muziki.

Hali hii bila shaka ilitokana na uwezo wa Nyashinski uliokubalika na watu wa rika zote kipindi kile alipokuwa kwenye kundi la Kleptomaniax ambalo liliundwa na vijana watatu ambao ni Nyashinski, Collo na Roba.

Watatu hawa walifanya vizuri katika miaka ya 2000 na walifanikiwa kuteka kila kitu na kulifanya kundi hilo kuwa kama kundi bora la Hip Hop Afrika Mashariki kwa kipindi hicho. Kwa kuzingatia kuwa Game la muziki tayari lililikuwa limebadilika sana ambapo kila uchwao wasanii wachanga wanaongezeka. Watu wengii hawakuutabiria mazuri ujio mpya wa Nyashinski huku baadhi yao wakidai alishasahaulika kabisa kwenye ramani ya muziki hivyo hawezi kurudi tena hata kwa kutumia nguvu ya ziada.

Mashabiki walishindwa kusubiri ili muda ufike ndio uonge wenyewe, msanii huyo alionekana kama mfa maji ambaye haishi kutapatapa. Wimbo huo ulipotoka mwezi wa February mwaka 2016 ulifanikiwa kupata mapokezi makubwa huku promotion yake ikiwa kubwa lakini pia kwa sababu ya uwepo wa Nameless kila kitu kilienda sawa, hiyo haina ubishi.

Licha ya hayo mapokezi bado haikueleweka wazi wazi iwapo Nyashinski alikuwa ‘serious’ kurudi kwenye muziki kwa kuwa alirudi tena nchini Marekani na kuendelea na mishe zake alizokuwa akifanya kipindi cha nyuma, hali hii ilionekana kuwachanganya mashabiki ambao walikuwa tayari wameshampokea kwa mara nyingine. Kumbe wakati wengi wakiwaza juu ya hilo msanii huyu tayari alikuwa na mpango na mwengine ambao unanifanya nimuone kama msanii mwenye upeo na akili nyingi sana, nitakueleza kwanini.

Aliitumia kolabo yake na Nameless kufanya ‘soundcheck’ na kuonyesha alama nyekundu kwa wasanii wenzake ambao labda walionekana wameliziba pengo lake.

Wakati huo huo mwezi April, ujio rasmi wa Nyashinski uliwakuta wengi kwenye mshangao. Aliachia wimbo wake uitwao ‘Know You Now’, ngoma hiyo ilisababisha gumzo kila kona ya Afrika Mashariki. Pia ilifanikiwa kuingia katika orodha ya ngoma zilizofanya vizuri mwaka huo kwa kipindi kifupi kwenye chati mbalimbali za runinga na radio lakini vile vile kupata mafanikio makubwa baada ya kupandishwa kwenye mtandao wa youtube tarehe 6 May, 2016.

Huu ndio ulikuwa mwanzo mzuri wa safari ya msanii huyo kwa kuachia ngoma kali kila kukicha, yaani ni mwendo wa bandika bandua. Aliumaliza mwaka kwa mshindo kikubwa kingine kwa kuachia ngoma kali ambayo iliwateka mashabiki wengi zaidi ‘Mungu Pekee’ ambayo ninaweza kusema ilibadilisha sura ya muziki wake kwa kiasi fulani.

Kwa maana kwamba ulikuwa wimbo wa kidunia lakini ulichukua mfumo na mantiki ya muziki wa injili na ukakubalika kila sehemu, hali ambayo ilisababisha mjadala mkubwa mitandaoni na pia kwenye vipindi tofauti tofauti vya burudani kuhusu aina ya wimbo huo ambapo mashabiki wengi walitaka utambuliwe kama wimbo wa injili na upewe nafasi katika vipindi vya dini.

Ulikuwa ni wimbo mkubwa sana ambao usipousikiliza lazima uuangalie. Video ya mashairi ya wimbo huo (Lyrics) katika mtandao wa YouTube imeweka rekodi ya kuwa video ya kwanza chini Kenya kutazamwa mara nyingi zaidi.

Haijatosha, mwezi wa April mwaka huu aliachia bomu jingine kwa kutoa nyimbo mbili ambazo zote zimekubalika na bado zinaendelea kufanya vizuri, hapa nazungumzia ‘Malaika’ ambayo hadi sasa imeangaliwa zaidi ya mara milioni 2 huku ‘Aminia’ ambayo nayo imetazamwa zaidi ya mara laki saba kwenye mtandao wa YouTube.

Kwa kifupi, msanii huyo tangu amerudi rasmi kwenye tasnia ya muziki nchini Kenya ameachia nyimbo nne kali ndani ya miezi 17, na ngoma zote hizo alizoziachiab zimefanikiwa kupata mapokezi makubwa pamoja na kufanya vizuri mpaka nje ya mipaka ya Kenya.

Hii inaonesha kuwa uwepo wake bado ulihitajika katika muziki na pia ni wazi kuwa ameweza kucheza vizuri na kuzipangilia ipasavyo hesabu zake zinazofanana na zile za ‘Magazijuto’ jinsi kitofauti kabisa na jinsi watu walivyotarajia.

Kwa hiyo, taarifa za Nyashinski kuteuliwa kuwania tuzo kubwa duniani za MTV Europe Music Awards 2017, kwenye kipengele cha Best African Act hazijanishangaza. Jitihada zake zimezalisha nafasi hiyo akiwa msanii pekee anayeiwakilisha ukanda huu wa Afrika Mashariki kwenye tuzo hizo ambazo zinatarajiwa kutolewa Novemba 12 ya mwaka huu mjini London.

Wasanii wengine ambao wanawania tuzo hizo katika kipengele hicho ni pamoja na Davido na Wizkid (wote kutoka Nigeria), Nasty C (Afrika kusini) na C4 Pedro (Angola). Mwaka uliopita tuzo hiyo ilinyakuliwa na Alikiba kutoka Tanzania na mwaka 2015 ilichukuliwa na Diamond Platnumz.

Hii ni nafasi nyingine tena kwa Afrika Mashariki kuja pamoja ili kuileta tena tuzo hii nyumbani. Ushindi wa Nyashinski ni ushindi kwa AfriKa Mashariki kwa ujumla kama walivyofanya wasanii wengine waliopita. Tuziweke pembeni tofauti zetu ushindi tunao

Bonyeza hapa kumpigia kura msanii Nyashinski.

Imeandikwa na: Ted Agwa
Instagram: @tedbway
+254710487436

Related Articles

Bongo5

FREE
VIEW