Nyerere akutana na Amin

Nyerere akutana na Amin
Watoto wawili wa viongozi wa zamani wa Uganda na Tanzania, Madaraka
Nyerere na Jaffar Amin, waliandika historia mpya baada ya kukutana
kwenye kijiji cha Butiama
alikozaliwa na kuzikwa Rais Julius Nyerere na kukubaliana kuanza umoja
mpya

 

Watoto hao, ambao baba zao walionekana
kuwa mahasimu wakubwa katika vita vya mwaka 1978 baina ya nchi hizo
mbili, walionyesha kusikitikia vita hiyo, huku mtoto wa Idd Amin wa
Uganda akisema "ilisababisha maafa makubwa" kwa wananchi wa Tanzania na
Uganda.

 

"Vita ile ilisababisha maafa makubwa kwa wananchi," alisema Jaffar
akionekana kusikitikia kitendo cha baba yake ambaye alikuwa chanzo cha
vita hiyo kwa kuishambulia Tanzania kabla ya Nyerere kuamua kujibu
mapigo kwa kuiondoa serikali yake madarakani.

 

"(Nyerere) ametuonyesha umoja, huyu ni bingwa wa suala hili. Mimi sijui
kabila lolote hapa Tanzania. Najua nyinyi wote ni Waswahili, lakini
kule kwetu wakiona wewe ni mrefu watasema ni kabila fulani, wakiona
mweupe kidogo, mwembamba watasema wewe ni Mnyankole.

 

"Lakini tangu wanajeshi wenu walipokuja kwetu, mnamwita kila mtu Mganda."

 

Jaffar, ambaye alikuwa akizungumza lugha ya Kiswahili, akiwa amevalia
kanzu ya bluu likiwa kama vazi la mitindo ya nchi za Afrika magharibi,
alitaka mkutano huo, ulioandaliwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza
(BBC), baina yake na Madaraka uwe mwanzo wa mshikamano baina ya
wananchi wa Tanzania na Uganda.

 

Mtoto huyo wa Idd Amin alienda kwenye kaburi alilozikwa Nyerere na pia
kutoa zawadi ya mkeka kwa mke wa muasisi huyo wa taifa la Tanzania,
Mama Maria Nyerere.

 

Naye Madaraka alisifu mkutano huo akisema umeongeza nia ya kuleta umoja.

 

Vita huyo ilidumu kwa miezi kadhaa na kufuatiwa na hali ngumu ya
kiuchumi kwenye nchi zote mbili, Tanzania ikitangaza kujifunga mkanda
kwa miezi 18 huku Uganda ikifuatiwa na mapinduzi mfululizo yaliyofikia
ukomo mwaka 1986 wakati Rais Yoweri Museveni alipoingia Ikulu akitokea
msituni.

Bofya hapa kusikiliza zaidi..

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents